HabariTravel

Watu wengine 21 wajeruhiwa katika ajali barabara ya Malindi – Mombasa…

Watu 21 wanauguza majeraha katika Hospitali kuu mjini Malindi baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani katika eneo la Kizingo kwa Mumba, barabara kuu ya Mombasa Malindi.

Kulingana na afisa msimamizi wa Hospitali hiyo Job Gayo,wanne kati yao wamevunjika miguu katika ajali hiyo iliyohusisha matatu mbili ambazo zimegongana ana kwa ana mwendo wa saa kumi na mbili unusu asubuhi ya leo.

Gayo ameeleza kuwa kati ya majeruhi hao,16 ni wanaume,wanawake wanne na mtoto mmoja huku akidokeza kuwa wahudumu wa afya wanaendeleza juhudi za kuwapa huduma za matibabu.

Kwa upande wake, Mary Harold,mmoja wa familia ya Mama aliyehusika katika ajali hiyo amesema mama huyo alikuwa ametoka Gede kuelekea Malindi kwa shughuli zake za kazi.

Mary anazidi kutoa wito kwa serikali kuharakisha ukarabati wa barabara hiyo ili kuzuia visa vya ajali kila mara.

Haya yanajiri siku chache baada ya watu 15 kupoteza maisha yao kufuatia ajali mbaya iliyotokea eneo lilo hilo.