AfyaHabariLifestyle

Faida Za Saumu….Sehemu Ya Tatu

Mfisada mkubwa ni mjuzi mwenye kupotosha (bila kujua) na aliye muovu zaidi ni mjinga mwenye (kupenda) ibada. Hao watu wa aina mbili hizi ni fitina kubwa kwa watu na hasa kwa mtu aliyeshikamana na dini kwa kuwafuata. Jee, vipi utamfuata mtu ambaye hajui?

Faida za kufunga ni nyingi sana tena mno, miongoni mwazo ni kutekeleza mojawapo ya amri za Mwenyezi Mungu Alizotufaradhia kwetu sisi na faida ya utekelezaji huu ni kuingia peponi.

Faida ya pili ya Saumu ni kujizoeza subira, yaani katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, mtu anajifunza jinsi ya kuweza kuvumilia na kustahamilia njaa, kiu, na kila matamanio ya kimwili. Mtume (s.a.w) amenena:

“Huo mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kusubiri, na hakika subira malipo yake ni pepo tu”.

Faida ya tatu ni kuwa na uadilifu na kujifundisha usawa baina ya tajiri na maskini.

Imam Ja’far As-sadiq (a.s.) alisema: “Hakika si jingine, Mwenyezi Mungu amefaradhisha kufunga ili wapate kulingana tajiri na maskini (katika shida ya njaa na kiu) basi akapenda viumbe vyake wawe sawa, na Amwonjeshe tajiri maumivu ya kushikwa na njaa ili apate kumhurumia mnyonge, na apate kumsikitikia mwene njaa”.

Faida ya nne na ambayo ni muhimu zaidi ni kughufiriwa katika mwezi huu na kusamehewa madhambi yote ya mwaka ikiwa mwenye kufunga ameyafuata masharti yote na kufunga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama alivyosema Mtume (s.a.w) katika mojawapo ya hotuba alizozitoa kwa minajili ya mwezi huu akasema:

“Enyi watu! Hakika umewaelekeni nyinyi, mwezi wa Mwenyezi Mungu (mwezi wa Ramadhani) kwa baraka, rehema na msamaha. Mwezi ambao ni bora mbele ya Mwenyezi mungu kuliko miezi yote, na siku zake ni bora kuliko siku zote, na masiku yake ni bora kuliko masiku mengine yote na masaa yake ni bora na muhimu kuliko masaa yote.”

By Yussuf Tsuma