HabariNews

MKUU WA IDARA YA DCI GEORGE KINOTI AMSHEREHEKEA DEVERA ALIYERIPOTI WANAFUNZI WATUNDU.

Hatimaye Mkuu wa DCI George Kinoti amekutana na dereva John Maina Muthoni ambaye aliripoti wanafunzi waliokuwa wanatumia mihadarati ndani ya matatu aliyokuwa anaendesha takriban wiki mbili zilizopita.
Kinoti amemkaribisha Muthoni ofisini mwake kufuatia mwaliko ambao alimpatia baada ya ripoti kuhusu kufutwa kazi kwake kuenea.
Muthoni anadaiwa kupoteza kazi yake ya dereva katika kampuni ya usafiri ya 2NK baada ya kuripoti wanafunzi 7 wa kiume na 7 wa kike ambao walikuwa wanavuta bangi na kubugia vileo ndani ya matatu walipokuwa wanasafiri kuenda nyumbani kwa kipindi cha likizo fupi.
Dereva huyo alielekea kituoni baada ya wanafunzi wale kumpatia vitisho alipowaonya dhidi ya kutumia mihadarati ile.
Kinoti amemsherehekea Muthoni kwa ujasiri ambao alionyesha huku akilaani kutimuliwa kwake kazini na akikashifu vikali kuongezeka kwa utumizi wa madawa ya kulevya miongoni mwa wanafunzi akisema kwamba kumechangia pakubwa kuharibika kwa maisha ya vijana wengi humu Nchini.