HabariNewsSiasa

Serikali ya Kaunti ya Kwale inashirikiana na Shirika la Aga Khan katika mradi unaolenga kuimarisha huduma za afya katika jamii.

Serikali ya Kaunti ya Kwale inashirikiana na Shirika la Aga Khan katika mradi unaolenga kuimarisha huduma za afya katika jamii.

Akizungumza alipopokea ufadhili wa vifaa vya matibabu kutoka kwa Shirika la Maendeleo la Aga Khan (Aga Khan Development Network) chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya EU, Gavana wa Kwale Fatuma Achani amepongeza ushirikiano uliopo baina ya shirika la Aga Khan na Serikali ya Kaunti akisema umesaidia pakubwa kupiga jeki huduma za matibabu katika hospitali na vituo vya afya Kwale.

Achani aidha amedokeza kuwa Serikali ya Kaunti ya Kwale itashirikina vyema na washikadau wote watakaojitokeza kupiga jeki juhudi za maendeleo katika Kaunti hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Aga Khan eneo la Mombasa Syed Mohammed Sohail, amesema kuwa ufadhili huo upo chini ya mpango unaolenga kuzisaidia Idara za Afya za Serikali za Kaunti katika kuimarisha huduma zao za matibabu na pia kukabiliana na changamoto zilizochangiwa na janga la Corona.

Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa leo na Shirika la Maendeleo la Aga Khan kwa Serikali ya Kaunti ya Kwale ni pamoja na vifaa vya maabara, vifaa vya kujikinga na maradhi ya Covid-19, na pia vifaa vya mafunzo kwa madaktari na wauguzi, vikiwa na thamani ya shilingi milioni 6.4.

BY EDITORIAL TEAM