HabariNews

SERIKALI YATAKIWA KUWAFUNGULIA MASHTAKA MADALALI WASIOZINGATIA SHERIA

Wito umetolewa kwa serikali kuwakamata na kuwafungulia mashtaka madali wasio na vibali wanaofanya kazi ya kuwasafirisha wasichana katika mataifa ya uarabuni kwenda kufanya kazi.

Kwa mujibu wa Alex Mwanza mtetezi wa haki za binadamu ukanda wa pwani kutoka shirika la Global Peace Intiative for the Poor, takriban wasichana 130 wamenusuriwa baada ya kupitia mateso kutoka kwa waajiri wao katika taifa la Saudi Arabia.

Anasema serikali inafaa kuweka mikakati ya kuwakamata madalali wanaojihusisha na biashara hiyo bila vibali vilivyothibitishwa na serikali ili kupunguza visa vya wasichana kutoka humu nchini kuteseka na hata kuuawa katika taifa hilo la Saudi Arabia.

Kwa upande wake Mary Charo mama wa watoto wawili na mwenye umri wa miaka 33, anasema alinusurika kifo mikononi mwa mwajiri wake baada ya kufungiwa kwenye chumba bila kupewa chakula kwa muda mrefu.

Ameeleza kuwa wakati wasichana hulazimishwa kuosha nyoka na kuwalisha, pamoja na kufanya kazi pasi kupumzika.

Aidha ametoa wito kwa wasichana wengine walio na azma ya kusafiri katika taifa la Saudi Arabia kufanya kazi kuachana na azma hiyo badala yake kutafuta kazi humu humu nchini.

Hata hivyo ameiomba serikali kuwatafutia kazi vijana ili kukabiliana na swala la vijana kuhatarisha maisha yao wakitafuta kazi katika mataifa ya uarabuni.

BY ERICKSON KADZEHA.