HabariNews

Kaunti ya Kwale Yatoa Ufadhili wa Milioni 10 Kwa Waliofeli KCPE 2023 Kujiunga na Vyuo vya Kiufundi

Wanafunzi ambao wamemaliza darasa la nane na hawakufanya vyema kwenye mtihani wao wa KCPE wameombwa kujiunga na vyuo vya kiufundi kaunti ya Kwale ili kukuza talanta za na ufundi.

Akizungumza mnamo Alhamisi huko Kingwede eneobunge la Msambweni, Gavana wa Kwale Fatuma Achani alisema kuwa serikali yake imetoa ruzuku ya shilingi milioni 10 kufadhili masomo ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivyo ambapo kila mwanafunzi atalipiwa shilingi 12,000 pindi atakapojiunga na vyuo hivyo.

Aidha gavana huyo alidokeza kwamba kufikia sasa kaunti ya Kwale imejenga jumla ya vyuo vya kiufundi 43 vinavyotoa mafunzo ya kiufundi mbali mbali yakiwemo mafunzo ya ujenzi, useremala, Utengezaji magari, mafunzo ya urembo pamoja na mafunzo ya uchumi wa baharini.

“Tumejenga vyuo 43 vya kiufundi katika kaunti yetu kutoa mafunzo kama ya useremala, ujenzi, urembo na hata uchumi samawati na isitoshe tayari milioni 10 ipo tumeitoa kufadhili watakaojiunga na vyuo hivi kusoma. Kila mwanafunzi tutamlipia elfu 12, nawahimiza hata mliofanya KCPE na hakumfaulu nafasi ipo na tutakupa ufadhili ujiendeleze,” alisema Bi. Achani.

Wakati uo huo Achani alieleza kutamaushwa na idadi ndogo ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivyo huku akiitaja idadi ya wanafunzi 4,000 pekee kuwa kidogo mno ikizingatiwa kwamba kaunti ya Kwale inapeana ufadhili wa masomo.

“Kaunti inatoa ufadhili lakini mbona msiichukue fursa hii? Wanafunzi elfu nne ni idadi ndogo sana nawahimiza wazazi tuwahimize vijana na watoto wetu kukumbatia elimu,” alisema.

Kauli yake iliungwa mkono na Mwakilishi Wadi ya Ramisi, Hanifa Mwajirani ambaye pia ni mjumbe anayewakilisha Walio wengi bungeni na alikuwa na haya ya kusema.

Kwa upande wake Naibu kamishna wa eneo la Msambweni Denis Juma aliwataka wazazi kujukumika ipasavyo na kutilia maanani masomo ya watoto wao.

BY BINTIKHAMIS MOHAMMED