HabariLifestyleNews

Serikali kutoa Shilingi Bilioni 1 kujenga upya Madarasa ya Shule Zilizoathiriwa na Mafuriko

Rais William Ruto amekariri mpango wa serikali yake kuwasaidia kwa msaada wa vyakula na mavazi kwa familia zilizoathirika na mafuriko nchini.

Rais Ruto mnamo Jumatatu Mei 6 alipowazuru waathiriwa wa mafuriko huko Kiamaiko eneo la Mathare kaunti ya Nairobi, alitangaza kila familia iliyoathirika kaunti hiyo itafidiwa shilingi elfu 10 kila mwezi kulipa kodi ya nyumba baada ya kuhamishwa kutoka maeneo hatari.

“Tumetambua familia 40,000 zilizoathiriwa na mafuriko Nairobi. Tutaipa kila familia KSh10,000,” alisema Rais Ruto.Alisema familia zilizoathirika zitapewa kipaumbele katika ugawaji wa nyumba 20,000 za bei nafuu, ambazo zitatangazwa hivi karibuni kwa ajili ya ujenzi.

Aidha Kiongozi wa taifa alisema Serikali imetenga shilingi bilioni 1 za kujenga upya madarasa yaliyoharibiwa na mafuriko kote nchini ili kuwakidhi wanafunzi pale shule zitakapofunguliwa tena.

“Kuna watoto wote wanaosoma shule zao zimaharibika. Nawatangazia serikali tumetoa shilingi bilioni 1 kujenga shule zenu upya tuhakikishe kila mtoto wa Kenya anarudi shuleni pale tutafungua shule wapate shule yao iko sawasawa ndio mtoto wa Kenya asikose mahali ya kusoma.” Alisema.

Aidha Rais alisisitiza dhamira ya serikali ya kupanda miti bilioni 15 ndani ya miaka 10 ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na athari za ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi.

“Tutashirikiana kwa karibu na mashirika ya kijamii katika kusafisha na kupanda miti kando ya Mto Nairobi,” Rais alisema.

Kufikia Jumapili Mei 5, Serikali ilikuwa imeripoti kuwa watu 228 wamefariki kutokana na mafuriko huku 164 wakijeruhiwa huku jumla ya familia 200,000 zikilazimika kuyahama makazi yao.

BY MJOMBA RASHID