HabariNews

Hakuna nafasi ya Uzembe na Kufeli Tena! Rais Awaonya Mawaziri

Rais William Ruto amewaagiza mawaziri kuwajibika vilivyo na kuzingatia sheria akisema uzembe hautakubalika tena.

Akizungumza baada ya kuongoza hafla ya kuapishwa kwa Mawaziri mnamo Alhamisi katika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto amesema Serikali yake haitavumilia tena watumishi wa umma wasiowajibika.

Kiongozi huyo wa taifa aidha amelikumbusha Baraza hilo kuwa limeanza rasmi oparesheni aliyoitaja kuwa haipaswi kufeli, huku akisisitiza kuwa matarajio ya Wakenya hasa vijana wa Gen Z ambao wameweka wazi kutovumilia utepetevu.

 “Viongozi hawa wa kike na kiume walioteuliwa kulihudumia Taifa katika Baraza lililoundwa upya leo wameanza misheni ambayo hawawezi na lazima hawapaswi kufeli.

Wakenya wameka matarajio yao peupe katika matakwa yaliyo wazi kabisa pia wameweka kutovumilia kufeli, kutowajibika, ufisadi bayana kwamba hawatayavumilia.” Alisema

Rais aidha ameahidi kuwa zimwi la ufisadi litaangaziwa na kukabiliwa ipasavyo akisema Baraza lake jipya aliloliunda litaangazia kwa kina suala la uwajibikaji, vita dhidi ya ufisadi serikalini na suala la kuondoa wafanyakazi hewa katika taasisi za umma.

Baraza lilioundwa upya litaangazia sehemu hizi muhimu, suala la uwajibikaji na uwazi katika vita dhidi ya ufisadi, kuondoa ulaghai wa wafanyakazi hewa katika viwango vyote vya serikali, na ili kufanikisha uwazi na uwajibikaji kwa matumizi ya raslimali za umma tutafanikisha uchunguzi wa haraka na kushtakiwa kwa wahusika wote wa kesi zinazohusu ufisadi na uhalifu wa kiuchumi.

BY MJOMBA RASHID