Kenya Harlequins ndio mabingwa wa Makala ya Sportpesa 7s 2024.Harlequins ambayo ndio timu yenye mafanikio zaidi tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo iliwazidi maarifa wanabenki wa KCB kwenye fainali ya kusisimua iliyosheheni patashika nguo kunachanika na nipe nikupe si haba baina ya miamba hao wawili.
KCB walipokonywa tonge mdomoni licha ya kutangulia mara mbili katika fainali hiyo na kusadikisha kauli kwamba kutangulia sio kufika.Ushindi huo wa alama 15-12 umeiweka timu ya Harlequins kileleni mwa msururu wa mashindano ya raga humu nchini huku wakita kibindoni kitata Cha sh 100000 nao wapinzani wao wakizoa sh 50,000 pesa taslimu.
Blak Blad nao walimtoa rangi bingwa mtetezi Kabras Sugar katika fainali za kuwania nafasi ya 3 kwa kuandikisha ushindi wa alama 22-7. Ushindi huo ulitia msumari kwenye vidonda vya wanakabras ambao walikuwa wangali wanauguza majeraha ya kubanduliwa kwenye nusu fainali na wanabemki wa KCB.Matokeo hayo yakiashiria kwamba mabingwa watetezi Kabras wataelekea nyumbani mikono mitupu huku Blak Blad wakivuna zawadi ya mshindi wa Tatu ya sh 25,000.
Katika matokeo mengine Daystar Falcons waliwashangaza wengi walipowazidi nguvu Strathmore Leo’s kwa alama 12-7 kwenye fainali ya kuwania nafasi ya tano huku Menangai Oilers wakidhihirisha weledi wao walipompiga Mwamba alama 14-0 kwenye fainali ya nafasi ya tisa, nao Nakuru Rfc wakaponyoka na ushindi wa alama 19-07 na kuyavunja matumaini ya Tum Marines ya kumaliza japo katika nafasi ya 13.
Katika mechi za Divisheni ya pili chuo kikuu Cha Kabarak hatimaye kilikwepa kisirani cha kupokonywa taji mikono baada ya kuwanyuka NYS Spades. Kabarak walifanikiwa kuhimili mashambulizi ya vijana hao wa NYS na kuponyoka na ushindi mwembamba wa alama 5-0 huku wakijishindia zawadi ya sh50,000 pesa taslimu.
Makala ya mwaka huu ya Sportpesa 7s maarufu pia kama driftwood 7s yaliyoandaliwa katika ukumbi u wa Mombasa Sports Club yatasalia kwenye kumbukumbu za mashabiki wa raga kwa muda mrefu kwani yalisheheni burudani,utashi na mechi za kusisimua zilizoshuhudiwa tangu kung’oa nanga kwa msururu huo siku ya Jumamosi.
BY MOHAMMED MWAJUBA