KWALE UNITED ndio mabingwa wa Makala ya mwaka huu ya Cheza Dimba na SportPesa yaliyoandaliwa Katika Uwanja Frere Ground Kaunti ya Mombasa.
Vijana hao Kutoka Kaunti ya Kwale walivuna ushindi huo mwembamba japo muhimu kwenye fainali baada ya Kuilabua na Kuichabanga AIC Kongwea Bao moja Kwa sufuri.
Mtanange huo wa kusimumua uliowaleta pamoja maelfu ya mashabiki, maashiki wahakiki na pia wakereketwa sugu wa soka kutoka Kaunti zote sita za Pwani waliofika kushuhudia Dimba hilo uliambulia sare ya Kutofungana kipindi cha Kwanza. Katika kipindi cha pili vijana hao wa Mama Fatma Achani walirejea uwanjani wakilenga kuvuna ushindi na haikuwagharimu muda mrefu Kabla ya kupachika bao hilo la Pekee kwenye Kipute hicho baada ya ngome ya Kongwea AIC kufanya masihara sadukuni.
Baada ya ushindi huo, Kwale United ilitia Kibindoni laki mbili unusu (Ksh.250,000) kutoka Kwa wadhamini wa Dimba hilo SportsPesa, jozi ya jezi za nyumba na ugenini pamoja na ufadhili wa miaka mitatu kutoka Kwa Kampuni hiyo ya Bahati nasibu.
Akizungumza Baada mtanange huo, Afisa wa masuala ya ushirikiano wa Umma Kampuni ya SportPesa Mercy Kabui alielezea kufurahishwa kwake na jinsi ambavyo Dimba hilo lilinoga na kuvutia halaiki ya watu uwanjani.
“Kwanza ningependa kuchukua fursa hii kuwashukuru mashabiki waliofika uwanjani kushangilia timu zao.Kwa Kweli mmefanikisha pakubwa Dimba hili. Pili, nashukuru pia timu zote zilizoshiriki dimba hili Ukanda wa Pwani, nidhamu imekuwa ya hali ya juu na tunashukuru Kwa ushirikiano wenu. Kwa mshindi wa Cheza Dimba Kwale United, Kongole sana kwao. Nina imani tuzo na zawadi ya laki mbili unusu na ufadhili watakaopewa vijana hao utawafaa pakubwa na utabadirisha maisha yao.” Alisema Mercy.
Aidha mercy alisema pamekuwepo na changamoto ya kupata timu ya kina dada ikijisali kushiriki Dimba hili jambo ambalo ameahidi Kuwa mwakani watahakikisha pamekuwepo na Dimba la timu za Kina dada.
“Kusema Kweli tumekuwa na changamoto Kupata timu ya wasichana imejisali kushiriki Tujiamini Cheza Dimba na SportPesa.Hata hivyo, tunaweka mikakati kuona mashindano yatakayoandaliwa mwakani yameshirikisha kina Dada pia.” Alisema Mercy.
Baada ya ushindi huo vijana wa Kwale United hawakuficha furaha yao wakisema Bidii ya kila mmoja wao ndio iliwapa ufanisi kwenye Dimba hilo Kauli iliyoungwa mkono na wakufunzi wao.
“Kwanza tunapongeza SportPesa Kwa kuandaaa Tujiamini Cheza Dimba. Hii ni mojawapo ya njia ya kukuza vipaji mashinani.Umoja na Bidii ya kila mmoja wetu ndio imeleta ufanisi katika Dimba hili.” Alisema Khalid Hamis.
Mbali na mtanange huo wa fainali, awali AIC Kongwea iliyofungwa fainalini iliipepeta Tiger FC kutoka Lamu 1:0 Kwa sufuri bao lililofungwa dakika ya 31 na Meshack Wambua.
Aidha Bam Bam FC ilitupwa nje ya Dimba hilo katika awamu ya nusu fainali ilipolabuliwa 1-0 na Kwale United Bao hilo la Pekee likifungwa na Matano Mwatondo dakika ya 5 ya Kipindi cha kwanza.
Awamu ya Robo fainali Rockside FC iliyaaga mashindano Mapema baada ya kufungwa bao moja Kapa na AIC Kongwea bao lililofungwa dakika ya 11 ya mchezo.
Wakati uo huo Frere Town FC maskini ilinyamazishwa nyumbani na Kwale United kwenye awamu ya Robo fainali baada ya Kulabuliwa mabao 2-0, mabao yaliyofungwa na Matano Mwatondo dakika ya 27 na pia 37 ya mchezo.
Kabla ya kuyaaga mashindano hayo rasmi, FRERE Town aidha ilikuwa imebamizwa 1-0 na Bam Bam FC bao hilo likifungwa na Francis Kadenge dakika ya 35 huku Tiger FC ya kutoka Lamu ikiichabanga Rockside FC mabao 2-0 kwenye mtanange wao wa kwanza, mabao yakifungwa na Francis Njoroge dakika ya 11 na Banard Maina dakika mbili badaye.
Ushindi wa Kwale United kwenye Makala ya mwaka huu ya Tujiamini Cheza Dimba na SportPesa yanaiweka timu hiyo kwenye madaftari ya kumbukumbu kama mojawapo ya timu ambazo zimeshinda taji la Dimba hilo la haiba Kubwa.
BY ISAIAH MUTHENGI