HabariNews

FAMILIA YA BARACK OBAMA YAJIPATA KATIKA MZOZO WA ARDHI KILIFI.

Familia ya aliyekuwa Rais wa Marekani Barack Hussein Obama imejipata katika mzozo wa umiliki wa kipande cha ardhi kule Jimba, eneo bunge la Kilifi Kaskazini kwenye kaunti ya Kilifi.

Mzozo huo unahusisha familia ya Obama na raia wa Ujerumani kwa jina Karin Gansfort anayedai kumiliki hati miliki ya ardhi hiyo ya ekari 3.2.

Kulingana na Gansfort ambaye pia ni mjane, aliuziwa ipande hicho cha ardhi mwaka wa 2007 na kupigwa na butwaa alipopata usajili wa cheti chake umefutwa na kupewa Rita Obama, dadake Rais Obama.

Aidha kwa mujibu wa stakabadhi katika afisi ya ardhi kaunti ya Kilifi, ardhi hiyo ilikuwa ya serikali kabla kusajiliwa kwa Lilian Uchi na Ndarewa Muyesi mwaka wa 2002.

Raia huyo wa Ujerumani sasa anatishia kuelekea mahakamani kutafuta haki na kujua nivipi ardhi hiyo ilipewa familia ya Obama bila yeye kujua, na nivipi cheti miliki chake kilifutiliwa mbali mnamo mwaka wa 2016.

Hata hivyo uchunguzi wa kituo hiki unaonesha kuwa raia huyo wa Ujerumani kupitia kwa kampuni yake amekuwa akilipia ada ya ardhi kwa kipande hicho cha ardhi tangu mwaka wa 2007 hadi 2018.

Kwa upande wake Rita Obama alithibisha kuwa na mzozo wa kipande hicho cha ardhi na kuagiza wakili wake kutoa taarifa zaidi.

Wakili wake Maurice Kilonzo hata hivyo amesema kesi aliyokuwa akimwakilisha Rita Obama ilihusu mpaka ambayo kwa ufahamu wake iliisha.

BY JOYCE KELLY MWENDWA