Bunge la kaunti ya Mombasa limepitisha mswada wa kufadhili mahitaji ya kimsingi ya watoto mayatima, walemavu na familia zisizojiweza katika wadi zote thelathini za kaunti ya Mombasa.
Akizungumza na waadishi wa habari baada ya mswada huo kupitishwa na wawakilishi wadi mnamo Jumanne Oktoba 3. Mwakilishi wadi ya Shanzu Allen Katana alipongeza hatua hiyo akisema ni jambo la busara viongozi kuwafaa wasiojiweza katika jamii wakati huu uchumi wa taifa umedorora.
“Nitoe shukrani kwa waheshimiwa wenzangu kwa kauli moja wote wameniunga mkono, ili watoto hawa mayatima na wanaotoka katika familia za watu wasiojiweza tuone ni vipi serikali yetu ya kaunti inaweza kuwaweka pamoja na kuwatimizia mahitaji mbalimbali muhimu,” alisema.
Mswada huo uliowasilishwa bungeni wiki iliyopita na Mwakilishi wadi wa Shanzu Allen Katana sasa unasubiri kutiwa sahihi na gavana wa Mombasa ndipo uanze kutumika kama sheria katika kufadhili masomo, makazi, malazi na mahitaji mengine ya kimsingi ya jamii hizo hasa kipindi hiki cha hali ngumu ya kiuchumi na kupanda kwa gharama ya maisha.
Wakati huo huo, Katana alimsuta Waziri wa Leba na Florence Bore aliyesema kwamba serikali kuu inapania kufunga makazi binafsi ya hifadhi za mayatima kwa madai ya ulanguzi wa watoto, akisema hatua hiyo huenda ikaleta matatizo zaidi badala ya suluhu la kudumu la changamoto wanazozipitia watoto mayatima nchini.
“Kwa hizi hifadhi za kibinafsi za watoto ni vyema zimilikiwe na serikali za kaunti, zitakuwa si za binafsi bali za serikali za kaunti ambazo zitafuatilia na kusimamia. Kwa bwana waziri akisema hifadhi zote zifungwe na hajatoa mbinu mbadala nasema si saw ana ni kukosa mwelekeo,” alisema Katana.
Kwa upande wake Susan Mwangi ambaye ni kiongozi wa kundi la kina mama la SIFA linalowahifadhi na kuwatunza watoto mayatima eneo la Shanzu amepongeza kupitishwa kwa mswada huo na kutoa wito kwa serikali ya kaunti ya Mombasa kukumbatia mswada huo ili kuwafaa wasiojiweza katika jamii.
Bi. Mwangi alitaka serikali kuhakikisha hifadhi zinazofungwa ni zile zinazokiuka sheria kwa kuwatumia watoto kama chambo cha kujipatia fedha na malengo mengine fiche.
“Kama mimi katika hifadhi ya watoto niko na watoto 300 na wako chini yetu je, ni wangapi wako huko nje hawako kwa hifadhi. Changamoto ni fedha na lau kungekuwa na fedha basi watoto wote wangekuwa wamefikiwa na kuwa kwenye hifadhi. Wito wangu ni serikali Kuu iangalie ni zipi wanafunga kama vitu vya mayatia vinavyokiuka sheria, sio kufunga vyote,” alisema.