Maafisa wa polisi mjini Mombasa wametibua maandamano ya walimu wanachama wa KUPPET waliokuwa wameanza mapema leo.
Walimu hao wa shule za upili walikuwa wamejitokeza eneo la Mapembeni kuanza maandamano yao waliyokuwa wameyapanga ili kushinikiza serikali ishughulikie matakwa yao.
Mamia ya walimu wanachama wa KUPPET walijitokeza eneo la Mapembeni mapema Jumatatu na kuanza maandamano yao waliyokuwa wameyapanga ili kushinikiza serikali ishughulikie matakwa yao.
Kinyume cha matarajio yao ya kuandamana hadi katika ofisi za Tume ya Kuajiri walimu TSC kaunti ya Mombasa kufikisha kilio chao, maandamano hayo yakatibuliwa na maafisa wa polisi waliokuwa tayari wamefika kuwazuia wasipige hatua mbele.
Idara ya polisi kaunti ya Mombasa kupitia Mkuu wa Polisi Maxwell Agoro imesema haikupokea barua yoyote kutoka kwa walimu hao kwamba wangefanya maandamano na hivyo basi hawakuwa na kibali rasmi cha kuandaa maandamano.
“Mliandika barua tarehe 24 mwezi huu (Agosti) na leo hii haijatimiza siku 3 inavyohitajika kisheria, imeandikwa kwenye sheria tafadhali tusilumbane, muandike barua ten ana mfuate sheria.” alisema Mkuu huyo wa Polisi.
Wakiongozwa na Naibu mwenyekiti wa KUPPET kaunti ya Mombasa Nelson Mandela walimu hao wa shule za upili wameikashifu hatua ya polisi kuwazuia kuandamana na kuitaja kuwa ukandamizaji wa haki yao.
“Walimu wa Mombasa leo asubuhi wamekuja kwa wingi tumeondoa huduma zetu shuleni kuja hapa kuandamana kuonyesha nchi nzima kuwa hatuezi kuendelea kuishi na mateso hapa nchini, tuliahidiwa bilioni 22 katika bima kutuasaidia sisi walimu lakini ukienda hospitali leo hii hakuna kitu hicho, hakuna chochote kinaendelezwa, tumesema haturudi shuleni!” Alisema.
Wakati uo huo walimu hao wamekashifu hatua ya wenzao wa chama cha KNUT kusitisha mgomo wao pasi maafikiano mwafaka kutoka serikalini.
Walimu hao sasa chini ya chama cha KUPPET, wanawataka walimu wenzao wasalie nyumbani huku wakiwahimiza wazazi kutowapeleka wanao shuleni.
“KNUT walitoa ilani yao ya kujiondoa kwenye mgomo wanadhani wanarudi kazini watalipwa na lakini hakuna kitu, walimu JSS wanateseka na lazima waajiriwe. Haturudi kazini hadi yatimizwe hayo, tunaungana na SG wetu na mwalimu yeyote shuleni tunakuja kukusalimia.”
Na huko mjini Hola kaunti ya Tana River walimu wanachama wa KUPPET wakiongozwa na viongozi wao wameandamana wakisisitiza kushiriki mgomo ulioanza huku wakisisitiza serikali isikilize kilio chao.
Peter Omondi ni Katibu wa KUPPET kaunti ya Tana River na ameongoza maandamano hayo na kukariri kuwa hawatarejea madarasani hadi pale Serikali itakapotekeleza matakwa yao.
“Waende watafute pesa kule watatafuta, kama walileta , CBA walitia saini wenyewe na wanakataa kutekeleza sasa, kisha wanaleta housing levy, wameleta NSSF, walimu ambao wamestaafu hawawezi kupata hata pensheni zao kwa hivyo hizi pesa tunawekezea nani?” Alisema.
“Tuko na machungu mengi hapa Tana River hata commuter allowance imekuwa shida hapa, tuna uchungu mwingi tukiwa nje ya darasa tunajua ni watoto wetu wanaumia lakini serikali inabidi itusikilize.”
By Mjomba Rashid