HabariNews

Vikao vya kutoa maoni havikufanyika ipasavyo Kilifi, tume ya kutetea haki za binadamu yasema

Shughuli ya kuandaa vikao vya kutoa maoni kuhusu mpango wa maendeleo wa mwaka 2025/26 wa serikali ya kaunti ya Kilifi imetajwa kutofanyika kwa njia ipasayo, madai ya maswali ya wakazi kukosa majibu yakigubika vikao hivyo vilivyotamatika Ijumaa wiki iliyopita.

Tume ya kutetea haki za binadamu nchini KHRC imetoa kauli yake kuhusu jinsi vikao vya kutoa maoni vilivyoendeshwa kaunti ya Kilifi juma liliopita.

Kulingana na Annette Nerima ofisa wa tume ya kutetea haki za binadamu, tume hiyo imethibitisha kukiukwa kwa kutotoa ilani ya siku 14 kabla kufanyika kwa vikao hivyo badala yake ilani iliyotolewa ni ya siku moja pekee.

Aidha ukosefu wa ufahamu wa kutosha kutoka kwa maofisa wa serikali waliokuwa wakiendesha vikao hivyo kunadaiwa kupoteza imani ya wakazi kuwa huenda wakatekelezewa miradi ambayo hawajaipendekeza.

 

“Tulipata kuthibitisha ya kwamba wananchi hawahusishwi jinsi ipasavyo wengi hawapatiwi notisi ya kutosha na tumekuwa tukipendekeza kwamba ukimpatia mwananchi wa kawaida notisi inafaa iwe ya siku 14 lakini tumethibitisha kuwa hii notisi inapeanwa ya siku moja.

“Na baadae tunaona hivi vikao vya kutoa maoni ikifanyika hawatumi wale maofisa wanaofaa ambao wataweza kujibu maswali ya wananchi wanatuma wale maofisa wa masomo ya nyanjani ama maofisa wa vyeo vya chini ambapo wakiulizwa maswali wanasema ngojeni tuende turudi na hawatawahi kurudi.” alisema Nerima.

 

Nerima ameongeza kuwa nakala za mpango wa maendeleo ya mwaka 2025/26 ya kaunti ya Kilifi zimekuwa zikifikishwa nyanjani siku ya vikao hali inayofanya wakazi kuwa na ugumu wa kuchambua nakala hizo na kutoa maoni yao kikamilifu huku akisistiza kuwa vikao hivyo vilifanyika ili kuondoa lawama bali sio kwa nia ya kupata maoni ya wakazi.

 

Na pia wanaleta zile stakabadhi zile za bajeti, zinaletwa siku hiyo hiyo ya vikao na mtu asiye mtaalamu si rahisi apate nafasi nzuri ya kuchambua zile stakabadhi za bajeti na kupata muda mzuri wa kutoa maoni yake.

“Kwa hivyo tutasema hivi vikao vya kutoa maoni vimefanyika ndio lakini serikali ya kaunti haijakusudia kukusanya maoni ya mwananchi kwasababu ingekuwa hivyo jambo la kwanza wangepatiwa notisi ya kutosha ili wapate kuchambua na maoni yao kuchukuliwa.” alisema Nerima.

 

Hayo yanajiri siku chache baada ya naibu gavana wa Kilifi Flora Chibule Mbetsa kuwahimiza wakazi kaunti ya Kilifi kuhakikisha kuwa wanatilia umuhimu swala la vikao vya kutoa maoni na kuhakikisha kwamba wanajitokeza kwa wingi wakati wa vikao hivyo.

 

Ninawaomba kina mama, baba, vijana na watoto wangu, huu ndio wakati wako wa kutoa maoni yako manake katika vikao hivi vya kutoa maoni mutaelezewa kuhusu miradi ambayo itakuja eneo lako. Je miradi hii mumeikumbatia? Je, ni miradi munayoitaka? Je, ipo katika miradi mnayoipa kipaumbele?

“Hatutaki tetesi zile zilizopita. Twasema yaliyopita si ndwele tugange yajayo lakini hii ndwele twaileta hatutaki zile rabsha za Gen Z kwasababu vikao vya kutoa maoni hawakuelewa kwa hivyo kukaja fujo.” alisema Chibule.

 

Erickson Kadzeha