Msako wa raia wa taifa la Afrika kusini anayehusishwa na visa vya ulawiti wa watoto wenye umri chini ya miaka 6 eneo bunge la Malindi ukiendelea, asasi za usalama kaunti ya Kilifi zimepewa makataa ya wiki moja kuhakikisha kuwa mshukiwa huyo mkuu wa ulawiti amekamatwa.
Viongozi, wanaharakati wa maswala ya jamii pamoja na mashirika mbali mbali ya kutetea haki za binadamu, wanaendelea kuzishinikiza asasi za usalama kumkamata mshukiwa mkuu wa visa vya ulawiti wa watoto eneo bunge la Malindi, Michael Ballentine anayeaminika kuwa mafichoni, wakidai kuwa jambo hilo ni ukiukaji wa haki za watoto.
Akitoa makataa hayo Mwakilishi wa Kike kaunti ya Kilifi, Gertrude Mbeyu amezitaka asasi hizo za usalama kutumia ujuzi wao kuhakikisha kuwa Ballentine anakamatwa mara moja, huku akizionya asasi hizo dhidi ya kutoa madai kuwa mshukiwa ametoweka nchini.
“Tutahakikisha ameshikwa, maana tunasikia amehepa nah ii Kenya huwezi kwenda pahali. Na tutaanza kwa kukamata familia yake kwasababu tunasikia yuko na familia hapa. Na tunapeana makataa ya wiki moja kufikia Ijumaa yule jamaa raia wa Afrika kusini awe amekamatwa.” alisema Mbeyu.
Mbeyu alisisitiza kuwa hatua za sheria zitachukuliwa dhidi ya wazazi ambao wamekuwa wakishiriki biashara hiyo, huku akieleza kuwa taifa la Kenya halitaruhusu vitendo vya kikatili kufanywa kwa watoto.
“Lakini mzazi ikiwa umehusika katika kupeana mtoto wako kwasababu ya shilingi elfu 2 mtoto wako wa miaka mitatu, miaka sita, tutakushika wewe ufunguliwe mashtaka uende jela miaka yako yote.
“Hatutakubali biashara kama hizi japo umaskini tuko nao ndani ya Kilifi lakini hatutakubali biashara ya watoto. Hatutaki haya yafanyike ndani ya Kilifi hatutaki yafanyike ndani ya Kenya.” alisema Mbeyu.
Hata hivyo mbunge wa Malindi Amina Mnyazi alitoa wito kwa wazazi kuwa waangalifu katika malezi ya watoto wao ili kuwaepusha watoto wao kupitia visa vya dhulma.
“Jamani tuchunge watoto wetu, usiamini mtu yeyote siku hizi, tumeelewana? Ikiwa hao wanawake wawili waliokamatwa wale wazazi waliwapa watoto wao wakijua hawa ni majirani hawakuwaona kuwa ni watu wabaya. Wanasema huyu mama ni mama mwenzangu tunakula pamoja, tunaishi pamoja, tunafanya kila kitu pamoja kumbe huku nyuma anakwenda kumuuza yule mtoto kwa shilingi elfu 2.” Alisema Mnyazi.
Mwanaharakati wa maswala ya Kijamii Wadi ya Kibarani, Khamisi Ali amesema hatua kali za sheria zinafaa kuchukuliwa kwa washukiwa ili kukomesha utalii wa ngono yaani “sex tourism”.
Aidha ameeleza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha maadili ya Kiafrika pamoja na kinyume cha misingi ya dini.
“Hivi vitu vimekithiri kaunti ya Kilifi kwa hivyo ningeomba zipigwe vita na ihakikishwe kuwa haitakubaliwa. Na nitaendelea kusema kwamba hatutaki kaunti ya Kilifi sex tourism isiweze kufanyika na mwisho nikimalizia hiki kitendo ni kinyume hata mbele ya Mwenyezi Mungu.” alisema Khamisi.
Ikumbukwe tayari washirika wawili wa Ballentine, Fatuma Mohamed na Nafisa Abdul Rashid, wamewekwa rumande huku kesi dhidi yao ikiratibiwa kutajwa tarehe Septemba 12, 2024.
By Erickson Kadzeha