HabariNews

JKIA Haitauzwa na Hakuna atakayeathirika; Isaac Mwaura 

SERIKALI haina nia ya kuuza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.

Ni kauli yake msemaji wa serikali Dkt. Isaac Mwaura akitetea hatua ya serikali kuigia kwenye makubaliano ya uwekezaji na kampuni ya miundomsingi ya India ya Adani.

Akihutubia wanahabari Mwaura amesema makubaliano hayo ya uwekezaji wa kima cha shilingi bilioni 242 (Dola bilioni 1.85) yanahusisha ukarabati wa mapaa yaliyozeeka na yanayojuja nyakati za mvua, na marekebisho katika uwanja huo sawia na kuupanua zaidi.

Hakuna atakayeathiriwa na uwekezaji huu hata hao ambao ni wafanyakazi hapa. Nawahakikishia kuwa hili litashughulikiwa vyema,” akakariri Mwaura.

Amesifia rekodi ya utendakazi ya kampuni ya Adani akisema ni ya kuvutia na hivyo ana imani kuwa itafanikiwa kubadilisha mwonekano na hadhi ya JKIA, huku akiwataka Wakenya kutokuwa na hofu kwani uwanja huo baadaye utarejeshwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Viwanja vye ndege nchini, KAA.

“Kwenda mbele tunatakiwa kubadilika na ndio maana tunahitaji mshirika mwenye mikakati na nasema hili pasi shaka kwamba Adani ana rekodi nzuri nchini India na maeneo mengine ya uwekezaji,” alisema Mwaura.

Mwaura aidha amewataka Wakenya kukaribisha wawekezaji wa kigeni kufadhili maendeleo ya taifa hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa uhaba wa fedha kusimamia miradi yake vilivyo.

Na mtaona mengi kama haya kwa kuwa tunahitaji uwekezaji kama huu wa kutoka nje ili kufadhili maendeleo yetu kwa sababu suala la kukopa limekuwa changamoto.” Alisema.

Haya yanajiri kufuatia shutma kali kutoka kwa Wakenya waliohisi kuwepo kwa mpango fiche katika suala hilo hasa baada ya serikali kushidwa kuweka wazi kwa umma kuhusu makubaliano hayo ya uwekezaji.

Mpango wa JKIA kukabidhiwa kampuni ya Adani umeratibiwa kufanyika mwezi Novemba 2024.

By Mjomba Rashid