Mshukiwa wa pili wa mauaji ya halaiki ya Shakahola kaunti ya Kilifi ameaga dunia akipokea matibabu.
Haya ni kulingana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma nchini, ODPP.
Inasemekana kuwa Edison Safari Munyambo maarufu Baba Sifa alifariki siku mbli zilizopita katika hospitali moja mjini Mombasa alikokuwa akitibiwa baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Munyambo ambaye anakuwa mshukiwa wa pili kufariki akiwa kizuizini baada ya Mary Charo Mbita aliyefariki katika Hospitali ya Rufaa ya Ukanda wa Pwani, Makadara, alikuwa miongoni mwa washukiwa 95 waliofunguliwa mashtaka 283 ya mauaji mbele ya Hakimu Mkuu wa Mombasa, Alex Ithuku.
Hakimu Ithuku hata hivyo amesema kulingana na ODPP kesi hiyo inapaswa kuendelea huku mahakama ikisubiri stakabadhi rasmi ya kifo cha mshukiwa huyo.
Itakumbukwa kuwa mshukiwa mkuu Paul Mackenzie na washukiwa wenza 94 wanaendelea kuzuiliwa wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwemo mauaji, mauaji bila kukusudia pamoja na kushambulia na kusababisha madhara.
By Mjomba Rashid