Hakuna hitilafu yoyote katika muunganisho wa nguvu za umeme ilijitokeza na kupelekea mkasa wa moto wa Endarasha.
Ni kauli ya Kampuni ya Umeme nchini Kenya Power, ikijitokeza kimasomaso kujitenga mbali na madai kwamba wanafunzi 21 wa shule ya msingi ya Hillside Academy kaunti ya Nyeri walifariki katika mkasa wa moto uliosababishwa na hitiliafu za umeme.
Katika taarifa yake mnamo Jumanne Septemba 10, kampuni hiyo imeondoa shauku na uwezekano wa kuwa mkasa huo wa moto ulisababishwa na kufeli kwa umeme, ikisema kuwa kila kitu kilikuwa shwari wakati wa mkasa.
Katika uchunguzi wao Kenya Power imesema wafanyakazi wake wamebaini kuwa usiku wa tukio hilo, laini ya kusambaza umeme shuleni humo ilikuwa imara na mitambo yote ilikuwa shwari.
Aidha Kenya Power imesema kuwa ilipopata habari za kuzuka kwa moto maafisa wake walichukua hatua ya kuzima usambazaji wa umeme kuelekea shuleni humo kama hatua ya mapema ya usalama, hivyo hakukuwa na vifaa vya umeme vilivyoathiriwa.
Haya yanajiri kufuatia madai na kauli za shahidi mmoja aliyesema moto huo ulisababishwa na hitiliafu ya umeme, huku mzazi mmoja ambaye mwanawe alinusurika mkasa huo akidai cheche za moto katika balbu karibu na mlango wa bweni ndizo zilizosababisha moto huo.
By Mjomba Rashid