Wakaazi wa Mombasa na Pwani kwa jumla sasa wanahimizwa kuwajibikia usafi wa mazingira sawia na upanzi wa miti ili kuimarisha mazingira yao.
Katika mahojiano ya kipekee na Sauti ya Pwani FM, katika hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja wa uboreshaji wa eneo la Splendid katikati ya jiji la Mombasa mnamo Jumamosi Novemba 23, Shujaa wa Mazingira Pwani Dkt. Mwinga Chokwe alisema upanzi wa miti unasaidia kuondoa hewa chafu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Hii miti tangu tuipande imekua na sasa inaleta kivuli kwa umma na pia inachangia mambo ya Carbon emission na climate change kupunguza global warming kwa sababu ya miti.” Akasema.
Dkt. Chokwe ambaye pia ni Mwenyekiti Kikundi cha Kijamii cha Clean Mombasa pia amewataka wakaazi pamoja na wafanyabiashara kaunti ya Mombasa kuwajibikia usafi wa mazingira yao ya kazi badala ya kusubiria huduma za maafisa wa kaunti pekee.
“Letu ni kuwaambia wakaazi wa Mombasa na wafanyabiashara waanze kuangalia mazingira yao wenyewe na pia ningewaomba kila jamii na kila eneo waliko wafanyibiashara washikane wasafishe wasingoje kusafishiwa na kaunti, kila mmoja awajibike.”
Wakati huo huo alisisitiza kuwa kuna haja ya serikali na mashirika husika ya mazingira kuelimisha jamii kwa jumla kuhusu umuhimu wa miti na mazingira safi.
By Mjomba Rashid