HabariNews

Wabunge 16 wa Tanzania Wajeruhiwa wakiwa safarini Kuja Mombasa kwa Michezo ya Bunge la EALA

Wabunge 16 wa Tanzania, wafanyakazi na dereva wamejeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuja Mjini Mombasa kwa Makala ya 14 ya Michezo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusika katika ajali.

Ajali hiyo imetokea mapema Ijumaa jijini Dodoma baada ya gari moja la mizigo kugongana na basi la wabunge hao.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma George Katabazi amethibitisha hayo akisema kuwa dereva wa gari hilo la mizigo anashikiliwa licha ya kuwa ni majeruhi.

Kulingana na taarifa iliyotolewa a Bunge la Tanzania majeruhi wote walikimbizwa katika hospitali mbalimbali mkoni Dodoma na kwamba hali yao inaendelea kuimarika vyema.

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula amethibitisha kupokea taarifa hizo akisema kuwa ni basi moja lilokuwa limewabeba baadhi ya wabunge limehusika katika ajali hiyo na kwamba hakuna vifo vilivyotokea.

Nimearifiwa kuwa basi moja lililowabeba baadhi ya wenzetu kutoka Tanzania lilipata ajali na hatuna vifo ila majeruhi kadhaa na wamekimbizwa hospitalini kutibiwa. Tunawatakia afueni ya haraka.” Alisema Wetangula.

Michuano hiyo inayoandaliwa maeneo mbalimbali Mjini Mombasa kuanzia Desemba 7 inajumuisha nchi 9 wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zikiwemo: Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Tanzania, Uganda, Sudan Kusini na taifa jipya katika Jumuiya hiyo, Somalia.

Michezo hiyo itajumuisha kabumbu, riadha, netiball, golfu, jugwe, miongoni mwa michezo mingine, itakamilika Disemba 18.

Michezo hiyo itafunguliwa rasmi Jumamosi, Desemba 7, katika ukumbi wa Mama Ngina Waterfront, huku Rais William Ruto akiongoza hafla hiyo.

By Mjomba Rashid