Wabunge na Maseneta wamesafiri kutumia reli ya SGR kutoka jijini Nairobi kuja mjini Mombasa kuhudhuria na kushiriki Makala ya 14 ya michezo ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula ametaja hatua ya viongozi hao kutumia usafiri wa reli ya kisasa ya SGR ni njia mojawapo ya kupunguza matumizi ya bunge.
Akizungumza na wanahabari kabla ya kuabiri treni hiyo mnamo Ijumaa, kuelekea mjini Mombasa Spika Wetangula ambaye aliongoza Wabunge na Maseneta alisema kuwa hatua hiyo ni mbinu mojawapo ya kuhakikisha fedha za ziada zinatumika katika masuala mengine ya maendeleo.
“Ukitumia ndege kama Spika ninalipiwa business class shilingi elfu 70 kwenda na kurudi, kwa SGR nafikiri tunalipa elfu 10 kwenda na kurudi, unaweza ukatafakari ni akiba kiasi gani tunayoweka na akiba hiyo itaenda kwa sekta nyingine za uchumi na kusaidia Wakenya wenzetu…” alisema.
Wetangula aidha alibaini ni lazima kama bunge kuwa kielelezo na mstari wa mbele katika kupunguza matumizi ya fedha za umma ambazo ni haba.
“Tunaenda na treni ya SGR kwa sababu tunajaribu kama wabunge kuonyesha nchi kwamba lazima tuwe mstari wa mbele kupunguza matumizi ya pesa ambazo ni chache katika nchi kwa mambo ya kazi yetu.” Alisema.
Michezo hiyo inayoandaliwa katika maeneo mbalimbali mjini Mombasa itajumuisha kabumbu, riadha, netiball, golfu miongoni mwa michezo mingine, itafanyika kuanzia tarehe 6 hadi 18 mwezi huu wa Disemba.
Michuano hiyo aidha inajumuisha nchini 9 wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiwemo Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Tanzania, Uganda, Sudan Kusini na taifa jipya katika Jumuiya hiyo, Somalia.
Michezo hiyo itafunguliwa rasmi Jumamosi, Desemba 7, katika ukumbi wa Mama Ngina Waterfront, huku Rais William Ruto akiongoza hafla hiyo.
By Mjomba Rashid