HabariNewsUncategorized

Jaji Lenaola wa Mahakama ya Upeo Aikosoa Serikali kwa Ulegevu katika kuunda upya IEBC

Jaji wa Mahakama ya Upeo Isaac Lenaola ameikashifu Serikali Kuu na Bunge kwa ulegevu wa kuunda upya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na badala yake kutanguliza sheria za kisiasa kwa gharama ya sheria zinazoathiri raia moja kwa moja.

Akizungumza baada ya kuhudhuria kongamano la kikanda kuhusu matumizi ya Akili mnemba (AI), kidijitali, na mitandao ya kijamii katika uchaguzi nchini KenyaJaji Lenaola aliisuta Serikali Kuu moja kwa moja kwa kushindwa kuunda tume hiyo kwa sasa, na kuibua maswali kuhusu hali ya sasa ya nchi bila makamishna wa IEBC, takriban miaka miwili tangu waondoke afisini.

Alilikashifu Bunge kwa kujishughulisha zaidi kupitisha sheria na masuala ya kisiasa na licha ya kuwa muhimu kitaifa, alisema kuna maswala muhimu zaidi kwa taifa hasa suala la kuundwa upya kwa tume hiyo ya uchaguzi.

Sielewi ni kwa nini, kwa mfano, tunafanya kazi ya kupitisha sheria haraka haraka kuhusu mambo mengine muhimu kisiasa, lakini hatuangalii ni nini muhimu sana kwa nchi hii – Tume ya uchaguzi. Vipi nchi kama yetu inawezaje kusimama imara ikiwa haina Tume ya uchaguzi?

Jaji huyo wa Mahakama ya Juu aaidha alihoji muda wa kushindwa kwa mfumo wa uwasilishaji kesi katika mtandao wa Mahakama wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya kumwondoa mamlakani aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na utayarifu wa mfumo kushughulikia mambo muhimu.

Mliofuatilia sakata la Riggy G mtakumbuka kuwa wakati fulani mfumo wa (Mahakama) wa kufungua faili la kesi mtandaoni uliharibika. Nataka mlibebe swali hili hadi 2027. Kwa nini jukwaa hilo la mtandaoni lilifeli? Fikiria nini kitatokea mwaka 2027.” Alihoji.

Jaji huyo sasa anawahimiza Wakenya kusimama na kushinikiza kuundwa upya kwa Tume uchaguzi ili kuwaruhusu kuafikia haki zao za kidemokrasia.

Mimi ni mmoja wa majaji ambao sina kikomo… nasema mawazo yangu… kwa nini tusitumie mitandao ya kijamii kushinikiza sheria? Kwa mfano, kwa nini hatuna hashtagi, #AppointIEBCNow, na kuisambaza? Wale walio na nafasi wataifuata na kusiambaza.

Kwa nini IEBC haiuindwi kwa sababu Azimio haiwezi kutaeua mwakilishi wake katia jopo, hilo ni suala la kuishikilia mateka nchi kwa miaka 2 bila IEBC kweli?

Hisia za Jaji huyo zinajiri huku shughuli nyinginezo zikiendelea nchini pasi uwepo wa makamishna wa IEBC, chini ya miaka mitatu kabla ya uchaguzi ujao, licha ya kuwepo kwa baadhi ya maeneo yanayokosa viongozi wawakilishi bungeni kutokana na uchaguzi mdogo kukosa kufanyika.

By Mjomba Rashid