Imebainika kuwa asilimia kubwa ya Wakenya huenda wanaugua magonjwa ambayo hawajui lolote kuyahusu; wengi wakigundua maradhi wakati hali ni mbaya zaidi au hakuna namna nyingine inaweza kufanyika.
Takwimu mpya kutoka kwa Wizara ya Afya, kitengo cha Idara ya afya ya umma na viwango vya kitaalam zimeonyesha taswira mbaya ya hali ya Wakenya waliopimwa na Maafisa wa Afya ya Jamii nyanjani (CHP) takwimu hizo zikiashiria kuwa Wakenya wengi ni wagonjwa wanaotembea.
Kulingana na takwimu hizo kati ya Wakenya milioni 22.5 waliopimwa ugonjwa wa kisukari kufikia sasa, zaidi ya 260,000 hawakujua wanaugua ugonjwa huo, achia mbali athari za kiafya zinazohusiana na ugonjwa huo.
Wakati uo huo utafiti huo ukibaini kuwa kati ya Wakenya milioni 15 waliopimwa shinikizo la damu, 577,000 wamepewa rufaa ya kwenda hospitali kwa matibabu maalum.
Fauka ya hayo Katibu Muthoni amebaini kuwa kati ya wanawake wajawazito 339,000 waliopimwa, takriban wanawake 132,000 hawakujali kamwe kuhusu kwenda kuhudhuria kliniki za wajawazito, na hivyo kuweka afya na ukuaji wa mtoto ambaye hajazaliwa katika hatari.
Mary Muthoni ni Katibu wa Afya umma nchini na anasema kuwa juhudi za kuimarisha afya nyanjani zimefanikishwa kwa ushirikiano wa maafisa wahamasishaji wa afya ya jamii (CHP) ambao hufika katika jamii mashinani kuelimisha na kuhimiza uzingatiaji wa afya.
”Huduma za CHPs zinaendelea vyema katika suala la usajili wa Taifa Care, shinikizo la damu, kuwaelekeza kina mama wajawazito na walezi kuhusu wakati wa kwenda kliniki,” Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni alisema huko Kibera mnamo Jumanne.
Muthoni anasema kuwa kuna tatizo na suala nyeti nchini ambapo watu hawazingatii afya zao kwa kuwa na shughuli nyingi za kutunza afya zao pasi kufahamu kuwa wanajiandalia mazingira magumu ya kufikwa na matatizo makubwa zaidi.
Wito sasa ukitolewa kwa Wakenya kutumia fursa ya likizo na sherehe hizi kutembela vituo vya afya kwa ukaguzi na kubaini hali zao za kiafya au kukumbatia huduma za Maafisa Wasimamizi wa afya ya jamii (CHP) kujua hali zao za kiafya.
Je, ni wakati gani hutembelea kituo cha afya kwa ukaguzi wa afya yako?
By Mjomba Rashid