HabariNews

Rais Awasihi Wakenya Kuwajibika na Kuzingatia Maadili mwaka Mpya huu 2025.

Rais William Ruto amehimiza umoja na uwiano katika kuliendeleza taifa na kukabiliana na changamoto zilizokumba nchi mwaka uliopita.

Katika hotuba yake ya Mwaka Mpya, huko Ikulu ndogo ya Kisii Rais amekariri suala la Wakenya kuwa na maadili na uwajibikaji mwafaka katika utendakazi wao ili kufanikisha umoja sawia na kukabiliana na chanagmoto za kimaadili.

Katika kile kinachoonekana kulenga vijana wakosoaji wa serikali ambao wamedaiwa kutumia mitandao vibaya, Rais amekariri umuhimu wa Wakenya na washikdau wote kuwa mstari wa mbele kulijenga taifa kwa msingi wa uzalendo, demokrasia na utawala wa sheria badala ya kuhujumu.

Vile vile Rais aliangazia maendeleo na changamoto za Kenya mwaka uliopita wa 2024, huku akielezea matumaini ya maendeleo kabambe mwaka huu wa 2025 na kuahidi kuendelea kuimarika na kukua kwa uchumi, kuongeza tija ya kilimo, uwekezaji na mageuzi imara ya sekta ya afya imara na elimu.

Licha ya changamoto kubwa, tulisimama pamoja, tulifanya kazi kwa dhamira, na kushinda vikwazo,” alisema.

Rais alimalizia hotuba yake ya Mwaka mpya kwa mtazamo chanya wa matumaini: “Pamoja, kwa umoja na azimio la pamoja, tutafanikisha Kenya Tunayoitaka.”

By Mjomba Rashid