AfyaHabariNews

Mgomo wa Maafisa wa Kliniki Wasitishwa kwa Muda wa siku 21

Muungano wa Maafisa wa Kliniki nchini, KUCO sasa umesitisha mgomo wao wa kitaifa kwa muda wa siku 21.

Hii ni kutokana na mazungumzo kati ya maafisa hao na wadau husika serikalini kuanza kutoa mwanga wa matumaini baada ya kujadili na kuafikiana kuhusu baadhi ya matakwa yao.

Katibu Mkuu wa KUCO, George Gibore amesema viongozi wa muungano huo wamefanya mazungumzo na Baraza la Magavana kuhusu malalamishi yao yakiwemo kutambuliwa na kujumuishwa kwa taasisi na maafisa wake katika mpango wa bima ya afya SHA.

Aidha Gibore amefichua kuwa lalama zao hizo pamoja na kuajiriwa kwa maafisa wanagenzi zinashughulikiwa, hatua iliyopelekea muungano huo kusitisha kwa muda mgomo wao ili kufanikisha utekelezwaji wa matakwa na malalamishi yao.

Hata hivyo Gibore amebaini kuwa mgomo huo wa maafisa wa kliniki ungali unaendelea katika kaunti za Kwale, Lamu, Vihiga na Uasin Gishu kutokana na masuala tata yanayohusu kaunti hizo.

Haya yanajiri huku Serikali za kaunti zikibaini kuhitaji muda zaidi kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na maafisa hao, hali iliyopelekea kutokubaliana kwa baadhi ya masuala hayo.