HabariMombasaNews

Pepo mchafu ashindwe! Magavana Wamsuta Mdhibiti wa Bajeti Kwa Kusitisha Ufadhili wa Basari za Kaunti

Huku mjadala kuhusu agizo la kusitisha ufadhili wa masomo wa kaunti ukiendelea kurindima, Magavana wanazidi kuibua pingamizi wakimshtumu Mdhibiti wa Bajeti Dkt. Margaret Nyakang’o ufuatia agizo hilo.

Wa hivi punde ni Gavana wa Kwale Fatuma Achani akimshtumu vikali Nyakang’o kwa kuzuia kaunti kutoa ufadhili huo, akisema ni sawa na kutaka wanafunzi waendelee kuteseka, kauli yake ikijiri baada ya Gavana wa Mombasa kutilia shaka agizo hilo.

Akizungumza huko Ramisi, Gavana huyo amesema kuwa huenda wanafunzi wanaotoka familia zisizojiweza wakaathirika pakubwa ikizingatiwa kwamba wamekuwa wakipata ufadhili wa karo kupitia mpango huo wa basari kila mwaka.

Ndani ya miaka yote aliyesoma vizui ni mtoto wa kitajiri pekee, tokea ugatuzi uingie mtoto wa maskini naye anasoma vizuri na pesa tunayopeana kama basari ndani ya jimbo hili imepitishwa kupitia vikao vya maoni ya umma. Leo hii Mdhibiti kukaa peke yake Nairobi kuondoa basari Kwale ni pepo mchafu huyo ashindwe.” Alifoka Achani

Aidha Achani amesema kuwa hadi kufikia sasa mpango wa Elimu ni sasa Kwale umefadhili masomo ya watoto zaidi ya elfu 8 waliojiunga na shule za upili za kitaifa, wanafunzi 6,000 wa vyuo vikuu na taasisi za kiufundi huku kila mwaka wanafunzi takribani elfu 16 wakinufaika na basari za kawaida na hivyo fedha za ustawishaji maneo bunge CDF zinazotolewa na wabunge hazitoshelezi mahitaji ya karo za wanafunzi wote wasiojiweza katika kaunti.

Kulingana na Achani, Kaunti ya Kwale hutenga jumla ya shilingi milioni 500 kila mwaka kufadhili masomo ya watoto hao hivyo kumtaka mhasibu huyo mkuu kubatilisha uamuzi wake huenda ukaathiri viwango vya elimu Kwale.

 “Inasikitisha sana kwa sababu tulipewa serikali ya majimbo ilikuwa ni sisi wenywe kujitawala tufanye kile tunataka kama kaunti, leo hii Mdhibiti wa bajeti akinambia serikali za kaunti zisifanye majukumu ya serikali ya kitaifa ilhali CDF wanazipa pesa kidogo sana. Pesa ya CDF itatosha kila mtu kaunti na kutulipia sote karo? Alisema.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Gavana wa Mombasa Abdulswanad Shariff Nassir kuendeleza cheche sawia za shutma kwa mdhibiti huyo wa bajeti kutoka na agizo lake hilo, akisema kuwa watafanya kila namna ikiwemo za kisheria ili kaunti zisalie na mpango huo wa ufadhili wa masomo.

Kuna mmoja Nairobi ameamua serikali za kaunti ati hazifai kulipia watoto wa sekondari, ni suala la kisheria na sisi tumesema kwanza tutaongea na yule mtu (Mdhibiti wa Bajeti) na njia ya pili tutatumia kisheria na kumwomba Mwenyezi Mungu amjaalie yule mtu abadili akili ajue kuna watu wenye matatizo na wanafaidika na basairi hizi.” Alisema Nassir.

Haya yanajiri huku wakazi wawili wa Mombasa, George Mwaura na Geoffrey Mugambi, wakiwasilisha kesi mahakamani kupinga agizo la mdhibiti wa bajeti Dkt. Margaret Nyakang’o la kusimamisha utoaji wa basari kwa wanafunzi wahitaji na serikali za kaunti, wakisema iwapo agizo hilo litatekelezwa basi wanafunzi wahitaji wataathiriwa pakubwa.

Jaji wa Mahakama kuu Jairus Ngaah aliipa kesi hiyo uzito wa dharura na kuwaelekeza kuwasilisha stakabadhi kwa Waziri wa Fedha John Mbadi, Mdhibiti wa Bajeti Dkt Margaret Nyakang’o na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor.

By NEWS DESK