Rais William Ruto amewatolea cheche za maneno wapinzani wake wanaompinga na kudai kuanzisha siasa na kampeini za mapema.
Kulingana na Ruto wanaomkosoa hawana ajenda nzuri kwa maendeleo ya taifa hili hasa kwa kudai kwamba Rais anafanya siasa kutokana na ziara anazofanya maeneo mbalimbali nchini.
Rais amekana kuzihusisha ziara zake na siasa za mapema akiwataka wapinzani wake kutoingiwa na hofu kwani wakati wa kufanya kampeini za kisiasa haujafika kwa sasa.
“…wacheni kuhara mapema siasa bado, sasa mnasema hii na siku tukianza siasa yenyewe si mtakimbia? Mimi niwaulize nyinyi mnaona tumeanza siasa sasa hawa watu waambie watulize boli, mambo bado, hii ni mambo ya maendeleo.” Akasema Rais.
Aidha akiwasuta kuhusiana na kiwanda cha sukari cha Mumias akisema wanaopinga hawana nia njema na wakulima na wakenya wanaojizatiti kuhakikisha wanajikimu kimaisha.
“Sasa mi nashangaa ati kuna viongozi wanauliza ati mbona serikali imesaidia kampuni ya Mumias mpaka imelipa bonus wakulima wa miwa, kwani mkuliwa wa miwa si Mkenya? Hawa watu wametembelewa na shetani na tuwambie washindwa kabisa.”
Vile vile, Ruto amemkashifu kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa madai ya ufadhili wa miradi mbalimbali aliyoizindua magharibi mwa Kenya.
“Yule Mtu wa katikati sijui watermelon ati ooh sijui hii pesa mmetoa wapi, ati anauliza maswali hii , kichwa yake ni mzuri ati anapinga. Mimi nataka nimwambie mtu ya watermelon mambo yakisimamiwa vizuri inaenda. Tumeweka proper management niliahidi tunaweka usimamizi sawasawa kuhakikisha sekta zinafanya kazi na tutawakomesha.” Akasema.
Ruto ameyasema haya akiwa katika ziara yake ya siku sita maeneo ya Magharibi mwa Kenya.
By Mjomba Rashid