HabariNews

Lilikuwa suala Dogo tu: Wizara ya Usalama wa Ndani Yakana Kuwepo Uhasama kati ya Serikali na Jaji Mkuu

Serikali imekana madai ya kuwepo uhasama na Jaji Mkuu Martha Koome wala Afisa yeyote wa Idara ya Mahakama.

Hii ni kufuatia utata kuibuka baada ya Jaji Mkuu huyo kupokonywa baadhi ya walinzi wake.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen amekana madai kwamba Jaji Mkuu huyo alipokonywa walinzi na badala yake walinzi wake watatu walichukuliwa baada ya kupandishwa cheo kupata mafunzo ya ziada.

Ilitubidi tulifanyie kazi suala hili, ili tuone jinsi tutakavyofanya kazi pamoja; kwa bahati mbaya, Jaji Mkuu wetu alijitokeza hadharani juu ya suala hili. Kwa ufafanuzi, CJ Koome alipaswa kumpigia IG kumshukuru kwa kuwapandisha vyeo maafisa lakini suala limekewenda kivingine kabisa,” Murkomen akasema.

Akizungumza katika eneo la Diani kaunti ya Kwale, Waziri huyo alibainisha kuwa Koome hakulazimika kufichua jambo hilo hadharani kwa vile limezua wasiwasi wa kimataifa kuhusu usalama wa Jaji Mkuu huyo.

Tunataka kumhakikishia Jaji Mkuu kwamba lilikuwa jambo dogo kulazimisha kuamsha wasiwasi. Watu duniani kote wanafikiri kuna mpango wa kukataa usalama wa CJ.”

Murkomen aidha alifichua kuwa Jaji Mkuu Koome bado amesalia na walinzi 29 ilhali katiba inamruhusu kuwa na walinzi 6 pekee.

Hata baada ya maafisa hao watatu kutumwa kwa mafunzo, CJ bado angebaki na maafisa 29; kulinda nyumba yake, usalama wa kibinafsi, hadi madereva kumi kati ya wengine,” akaongeza.

Waziri huyo hata hivyo amemhakikishia usalama wa kutosha Jaji Mkuu Koome na maafisa wengine wote wanaostahili walinzi kuwa watapewa ulinzi kulingana na katiba na kwamba serikali haitavunja kanuni hizo.

By Mjomba Rashid