Siku chache tu baada ya chama cha Amani National Congress (ANC) na kile cha United Democratic Alliance (UDA) kuungana na kutangaza kuundwa kwa chama cha United Democratic Alliance Party, Katibu mkuu wa ANC Kaunti ya Mombasa Athman Ali Abdalla Almaarufu Athman Timberland amesifia ndoa kati ya vyama hivyo viwili akisema itakuwa yenye heri na Manufaa kwa wakaazi wa Pwani na Kenya Kwa Jumla.
Akizungumza na Sauti ya Pwani Fm katika kipindi cha Gumzo Pevu, Athman amekariri kuwa ushirikiano wa chama cha ANC chake waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi na chama tawala cha UDA cha Rais William Ruto utadumu kwa muda mrefu kwa mujibu wa Muktaba wa maelewano wa kisiasa kati ya vyama hivyo viwili.
“Sisi ANC ni waandani wa kwanza na washirika wa karibu katika serikali ya Kenya Kwanza.Hatuwezi kuepukana na UDA. ANC itakufa na UDA hata ikijaribu kutukimbia bado kuna mahali tutakuwa tumeshikana.” Alisema Athman
Katibu huyo wa ANC kaunti ya Mombasa ambaye pia ni mwekahazina wa chama hicho Ukanda wa Pwani amesema kuwa baada ya ANC kujiunga rasmi na UDA huenda vyama vingine tanzu vya muungano wa Kenya Kwanza ambavyo vimekataa na kujivuta kuungana na chama hicho tawala vikalazimika kufuata mkondo siku za hivi karibuni.
“Kuna uwezekano mkubwa kwamba vyama vingine vitafuata mkondo wa ANC na vile ambavyo havitafanya hivyo vitakuwa vinalemaza na kuyumbisha ajenda ya rais na serikali yake.Hii Kenya lazima tuunganishe ikuwe kitu kimoja. Sisi ANC tumejiunga na UDA, Ford Kenya na PAA itakuwa inaungana nasi hivi karibuni na vyama vingine kadhaa.Hata hii ODM tutaishawishi na hatimaye huenda ikajiunga nasi baadaye.” Alisema Timberland.
Rais William Ruto amekuwa akisisitiza kuwa vyama tanzu 18 vya muungano wa Kenya Kenya vinapaswa kuvunjwa ili kuunda chama kimoja chenye nguvu, wito ambao umekuwa ukipingwa na baadhi ya vyama hivyo.
Mnamo Ijumaa, UDA na (ANC) vilikamilisha mchakato wa kuungana na kutangaza kuundwa kwa chama cha United Democratic Alliance Party ambacho kitakuwa na alama na rangi zinazoakisi vyama hivyo viwili.Mwenyekiti wa UDAP, Cecily Mbarire alisema hatua hii ilijiri baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo.
Kwa upande wake Issa Timami aliyekuwa mwenyekiti wa ANC, atakuwa naibu kiongozi wa chama kipya. Makamu Mwenyekiti wa chama hicho atakuwa Kelvin Lunani, huku Naibu Katibu Mkuu akiwa Omboko Milemba.Kulingana na Mbarire, shughuli ya kuunganisha vyama hivyo viwili ilianza mapema mwaka jana lakini ikalazimika kukwama kufuatia msukosuko na changamoto zilizokuwa zikikabili chama tawala.
Baadhi ya vyama ambavyo huenda vikakumbana na dhoruba la shinikizo ni kile cha Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ambaye chama chake cha Ford Kenya kimekuwa kikijivuta kumezwa na UDA na mwenzake wa Seneti Amason Kingi aliyeongoza chama cha Pan African Alliance (PAA) kujiunga na Kenya Kwanza.Wengine ni Alfred Mutua wa chama cha Maendeleo Chap Chap ambaye ni waziri wa Leba na mwenzake wa Utumishi wa Umma Justin Muturi anayehusishwa na chama cha Democratic Party na Mwangi Kiunjuri wa chama cha The Service Party.
Kadhalika chama cha Mashinani ambacho kinahusishwa na aliyekuwa gavana wa Bomet Isaac Ruto anayehudumu katika Tume ya Huduma ya Mahakama, Tujibebe Wakenya Party ambacho kiongozi wake William Kabogo aliteuliwa waziri wa ICT na Uchumi Dijitali. Aidha, Farmers Party cha aliyekuwa katibu wa wizara Irungu Nyakera na United Democratic Movement kinachohusishwa na seneta wa Mandera Ali Roba miongoni mwa vingine.
Mwaka jana, wakati ANC ilipotangaza ilikuwa ikizungumza na UDA kuelekea muungano ambao ulikamilika jana, Katibu Mkuu wa Ford Kenya John Chikati alisema chama hicho chenye alama ya simba hakitavunjwa.
“Kumekuwa na uvumi kwamba vyama vinavunjwa. Kwanza, hakuna mtu aliyekuja kwetu kutuomba tuvunje chama chetu. Hata kama wangetuuliza, Ford Kenya hawawezi kuvunjwa.Tutaendelea kuwepo.Baadhi ya vyama ibuka vitaondoka na kuacha Ford Kenya uwanjani. Hatutavunja chama, tunaweza tu kukipanua na kuacha chama hiki kwa kizazi kijacho,” alisema Chikati, baada ya mkutano wa kamati simamizi ya chama mwaka jana.
Huku Rais William Ruto akirajiwa kuzuru ukanda wa Pwani hivi karibuni Athman Timberland amesema ziara hiyo itakuwa manufaa na natija tele kwa wakaazi wa Pwani.Kulingana na Athman, Rais William Ruto katika ziara yake anatarajiwa kuzindua miradi kadhaa ukanda wa Pwani inayolenga kuwananufaisha wakaazi wa eneo hilo.
“Rais akija mwishoni mwa wiki inayokuja ataleta miradi kadhaa na kufungua viwanda vitakavyotoa nafasi za ajira kwa wa Pwani .Hii miaka miwili ni ya kazi tu.Rais ana nafasi ya kurekebisha alipofeli miaka miwili iliyopita. Viwanda vya korosho Kilifi atavishughulikia na Pia Basetitanium yak wale ataivalia njuga. Nawaomba wakenya tuwe na subira na serikali hii, mambo mazuri yanakuja.” Alisema Athman Timberland.
Ziara ya Rais William Ruto ukanda wa Pwani inajiri huku uteuzi wa Ali Hassan Joho kama waziri wa madini na Salim Mvurya kama waziri wa michezo ukitarajiwa kuwa msingi wake wa kupenya ngome ya ODM ambayo kwa muda mrefu imekuwa himaya ya Raila Odinga.
Kuhusiana na mustakabali wake wa kisiasa, Athman Ali Abdalla anakiri kuwa atakuwa anajitosa debeni mwaka wa 2027 kuwania wadhifa wa kisiasa kwa mara ya tatu, baada ya juhudi zake za kuwa mwakilishi Wadi eneo la Old Town – Mji wa Kale kugonga mwamba katika uchaguzi mkuu uliopita.
BY ISAIAH MUTHENGI.