Grace Njoki, mmoja wa wanawake waliokatiza kikao cha Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa kwa ujasiri katika Jumba la Afya House wiki iliyopita, ameeleza masaibu aliyopitia baada ya kukamatwa kwake na maafisa wa polisi katika hospitali ya Ladnan jijini Nairobi.
Akizungumza na wanahabari katika Kituo cha Polisi cha Capitol Hill jijini Nairobi muda mfupi baada ya kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu ya shilingi 10,000 ameeleza kuandamwa na kufuatilia na maafisa hapo awali ambao walimkamata na kumzungusha katika vituo vitatu tofauti vya polisi.
“Nilikuwa nimeenda kutafuta matibabu katika Hospitali ya Ladnan na nilimuona mtu wa usalama ambaye nilimuona hapo awali na hata nikamuuliza alikuwa anafanya nini huko. Ninaweza kumtambua hata ninapomwona,” Njoki alisema.
“Kwa hiyo, nilihisi nilikuwa nikifuatwa”
“Alitokea kusikojulikana na kunisalimia hivyo nikamwambia nimekuja kuchukua majibu yangu kwa sababu waliniuliza nilikuwa nafanya nini hospitalini. Alidai alikuwa na mgonjwa,” alisimulia.
Dakika chache baadaye, Njoki alisema afisa huyo alirudi akiwa na mwanamume na mwanamke, labda wenzake na kumtaka aondoke nao hospitali.
“Haikupita dakika 10, alirudi na mwanamke na mwanamume na kuniambia wanataka kunipeleka mahali fulani. Niliuliza nimefanya nini na wananipeleka wapi lakini walikataa kuniambia
“Pia walikataa kunieleza kwa nini nilikuwa nikikamatwa, wakidai kuwa sikuwekwa chini ya ulinzi,” alisema.
Grace Njoki alisema kuwa mpaka kufikia sasa hajajua sababu ya kukamatwa kwake.
“Nilihisi kutekwa nyara kwa sababu hiyo ndiyo ilikuwa hofu yangu. Sijui kwanini nilikamatwa kwangu haikuwa kukamatwa, ilikuwa ni kutekwa. Je, hawawezi kuningoja nimalize matibabu yangu?” alisema.
Wanajua mahali ninapokaa, waliniambia hata wanaijua nyumba yangu … hawawezi kunipigia simu kwa sababu walikuwa na nambari yangu? Si haki kunishughulikia wakati nikitafuta matibabu.” Akaongeza.
Fauka ya hayo, Njoki alieleza kwa moyo mkunjufu kwamba hatua yake ya kuvamia mkutano wa Waziri Barasa ilitokana na nia yake ya kupigania haki za wagonjwa, kwa kuwa Mamlaka ya Afya ya Kijamii, SHA haina ufanisi na inaweka afya ya Wakenya hatarini.
“Nimekuja tu kupigania wagonjwa ambao hawana sauti. Mimi si kiongozi wa kisiasa. Sitafuti kitu; Mimi ni muuguzi na watu wote wanaonifahamu, nimekuwa nikipigania wagonjwa kila wakati,” akasema.
Kwa upande wake Ndegwa Njiru ambaye ni wakili humu nchini amesema kuwa ni wakati sasa kwa mawakili wote nchini kujitokeza na kupigania haki za wakenya wakitarajia Grace kupelekwa mahakamani ili ukweli kujulikana.
By News Desk