HabariNews

Ripoti ya FKE Yabaini Zaidi ya Wakenya 5,000 walipoteza kazi, kampuni 57 zikifuta watu Kazi Tangu mwaka 2022

Shirikisho la Waajiri nchini (FKE) limeibua wasiwasi kuhusu Serikali kuendeleza makato zaidi ya ushuru wa Wakenya katika juhudi za kuongeza mapato zaidi ya ushuru ili kufadhili matumizi.

FKE inasema hii inaweza kusababisha machafuko ya kijamii huku Wakenya wengi wanaolipwa wakihisi kutoridhika chini ya shinikizo linaloongezeka la kuendeleza maisha yao kwa kupungua kwa malipo yao wanayosalia nayo baada ya makato.

Waajiri hao wanaonya kuwa malipo ya Wakenya wanayosalia nayo kwenda nyumbani yamepunguzwa hadi chini ya theluthi moja iliyopendekezwa.

Kulingana na FKE, tangu kuanzishwa kwa ushuru mpya na makato, waajiri wanapata ugumu kuzingatia sheria, huku wengine wakikata zaidi ya mahitaji ya sheria.

Waajiri hao pia walifichua kuwa chini ya utawala wa sasa, tangu 2022, karibu watu 6,000 wamepoteza kazi zao, na angalau kampuni 57 zilitangaza kuwafuta kazi.

Ni wazi tukiendelea kuvamia hati ya malipo hatutakuwa na kipato. Kwa hiyo watafanya nini? Watalazimika kuendelea kukopa; watahangaika, na hatimaye kuleta machafuko ya kijamii. Kisha watu wanaanza kujiuliza ni nini thamani ya kuajiriwa,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa FKE Jacqueline Mugo katika taarifa.

Licha ya changamoto hizo, FKE ina matumaini kwamba 2025 inaweza kuwa mwanzo wa uimarishaji wa uchumi, mradi marekebisho muhimu ya sera yatafanywa ili kupunguza shinikizo la kodi na udhibiti linalolemea biashara na wafanyikazi kwa sasa.

By Mjomba Rashid