FunGamingHabariMombasaNews

Sayani FC, Mabingwa wa Kijiji cha Takaungu

Sayani FC wametawazwa mabingwa wa kijiji cha Takaungu baada ya kuwabamiza FC Madrid kwa bao moja bila jibu kwenye mtanange wa TK Derby.

Sayani FC wamepata haki ya kujigamba baada ya kuibuka mabingwa kwenye mchuano wa TK Derby baada ya bao la Komora Khamisi mnamo dakika ya 19 kuwapa ushindi katika mchuano huo.

Kwa mujibu wa mkufunzi wa Sayani Safari Baya, wanalenga kuweka mazingira bora yatakayowezesha vipaji vichanga kukuwa na kupata nafasi ya kucheza mpira katika ngazi za kimataifa na hata kuiwakilisha timu ya taifa Harambe Stars.

Mchezo wa leo umekuwa vizuri. Vijana wa Sayani wameonesha kiwango bora kimchezo licha ya kuwa nimeanza kuwafunza siku chache zilizopita. Na nimewaambia hawa vijana twende tucheze mpira wala sio kwa kujionesha na hakika wamefuata maagizo na tumepata ushindi. Ningependa kuwasistiza wachezaji wajizatiti ili kuimarisha viwango vyao vya mchezo ili waweze kufikia viwango vya kimataifa.” alisema Baya.

Kwa upande wake Morris Eliud mkufunzi wa FC Madrid ameeleza kufurahishwa kwake na viwango vya talanta zinavyojitokeza kupitia michuano ya mashinani, akitoa wito kwa viongozi na wahisani kuwekeza vilivyo kwenye vifaa na viwanja vizuri ili kukuza vipaji hivyo.

Ameongeza kuwa vijana kushiriki michezo kunawaepusha kujihusisha na utumizi wa dawa za kulevya pamoja na maswala ya uhalifu.

Mchezo ulikuwa mtamu sana kwa timu zote mbili, mchezo huu umeonyesha wingi wa talanta tulionao mashinani. Kiwango cha kandanda hapa kwetu kiko kiwango cha wastani kwasababu wengi hawana uzoefu kwa kuwa hatujashiriki ligi kwa muda mrefu. Basi natoa ombi kwa viongozi na wahisani waweze kutusaidia na vifaa vya kufanyia mazoezi na pia watusaidia kuweka tambarare uwanja wetu na kututengenezea viwanja vingine ili hivi vipaji vikuzwe kwa njia bora. Vijana wakijishughulisha na maswala ya michezo hawatakuwa na muda wa kufikiria kufanya uhalifu wala kutumia mihadarati.” alisema Eliud.

Diwani wa Mnarani Juma Chengo, ameeleza kuwa kwa ushirikiano na wadau mbali mbali kama vile Imtiaz Sayani wameanza mpango wa kusaka na kuibua talanta kutoka mashinani na kuwaunganisha na maskauti wa vilabu vikubwa ili kuwasaidia vijana hao kufikia viwango vya kuwa wachezaji wa kulipwa.

Kwa ushirikiano na Imtiaz Sayani tuna mipango ya kuanza mashinani kama vile ambavyo tunafanya saa hii tupate ile timu bora na kisha tutakuwa tunazungumza na maskauti wa vilabu vikubwa vikubwa hapa Kenya ili waweze kubaini ni talanta zipi wangependa kufanyakazi nazo na kufikia kuwa wachezaji wa kulipwa.” alisema Chengo.

Mshindi wa ngarambe hiyo ametuzwa kombe na shilingi elfu 10 pesa taslim huku mshindi wa pili akitia kibindoni shilingi elfu 5 pesa taslim.

Na Erickson Kadzeha.