Nafasi ya Raila Odinga kunyakua Uenyekiti wa Tume ya Afrika, AUC imepata kitisho baada ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kutangaza kuunga mkono mgomea wa Madagascar.
Jumuiya ya SADC inayojumuisha nchi 16 wanachama, imewataka wanachama wake kumuunga mkono mgombeaji wa Madagascar Richard Randramandiato katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) unaotarajiwa kufanyika Jumamosi, Februari 15.
Hatua hii ya dakika za mwisho inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mgombea wa Kenya, Raila Odinga, ambaye amekuwa akitegemea kuungwa mkono na mataifa ya SADC ili kuimarisha nafasi yake dhidi ya wapinzani wake wakuu wawili-Mahamoud Ali Youssouf wa Djibouti na Richard Randriamandrato wa Madagascar-katika uchaguzi huo wa hali ya juu.
Katika barua yake ya Februari 12 iliyotumwa kwa nchi wanachama wake, Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi, alithibitisha ombi rasmi la Madagascar la kuungwa mkono kikanda, akisisitiza kuwa Randriamandrato anasalia kuwa mgombea pekee kutoka jumuiya hiyo.
“Ninakuandikia kukujulisha, Mheshimiwa Waziri, kwamba Mheshimiwa Richard J. Randriamandrato, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Madagascar, ameorodheshwa kuwa mgombea pekee kutoka kanda ya SADC kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika,” Magosi alisema.
Alieleza zaidi kwamba, kutokana na muda mfupi kabla ya uchaguzi, hakuna haja ya kuitisha Baraza la Mawaziri la Kigeni kujadili ombi la Madagaska, badala yake, barua ya sekretarieti ya kutaka kuungwa mkono kikanda ingetosha.
“Kwa kushauriana na Mwenyekiti wa Baraza, na kutokana na muda mfupi kabla ya uchaguzi wa Mwenyekiti, hakuna haja ya kuitisha Baraza la Mawaziri la Kigeni ili kuzingatia ombi la Madagaska. Barua kutoka kwa Sekretarieti ya kutaka Nchi Wanachama wa SADC kuunga mkono kugombea Madagaska inapaswa kutosha.”
Nchi 16 wanachama wa SADC ni pamoja na Angola, Botswana, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia, na Zimbabwe.
Wakati huo huo, Rais wa Kenya William Ruto aliwasili Addis Ababa siku ya Alhamisi kuhudhuria Mkutano wa 38 wa Kawaida wa Umoja wa Afrika, ambapo wakuu wa nchi watapiga kura zao kumchagua Mwenyekiti na Naibu Mwenyekiti ajaye wa AUC.
Chini ya sheria za AU, upigaji kura unafanywa kwa kura ya siri na itaendelea hadi mmoja wa wagombea apate uungwaji mkono wa thuluthi mbili ya nchi 55 wanachama wa AU, ambao ni kura 33.
By Mjomba Rashid