Kadri ulimwengu unavyoendelea kupiga hatua kiteknolojia, idadi ya vijana wasio na ajira ndivyo inavyozidi kuongezeka.
Katika maeneo mengi ukanda wa pwani na kote nchini, kuna mtazamo unaokua miongoni mwa vijana kwamba mafanikio yanaweza kupatikana tu kupitia ajira rasmi za ofisini. Kutokana na dhana hii, wengi hupuuza kazi za mikono, wakiziona kuwa ngumu na zisizo na heshima kwao. Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya teknolojia na digitali ulimwenguni, mtazamo huu unabadilika, na uhitaji wa kazi za mikono zenye ujuzi unaongezeka kwa kasi. Ummi Sora, msaidizi katika shirika la I.O.ME 001,chini ya shirika la Msalaba Mwekundu (Kenya Red Cross), aliwahimiza vijana kuachana na mtazamo wa kutegemea ajira za ofisini na badala yake wakumbatie kazi za ufundi kama fursa za ajira.
“Ni wakati wa vijana kuthamini kazi za mikono. Kazi hizi zimepuuzwa kwa muda mrefu kwa sababu ya imani kwamba ni ngumu. Hata hivyo, hizi ndizo kazi zinazohitajika sana sokoni. Kwa kuwa na ujuzi sahihi, mtu anaweza si tu kujiajiri, bali pia kuajiri wengine,” alieleza Sora. Aliendelea kueleza kuwa kuna nyanja nyingi zenye fursa kubwa kwa sasa, kama vile useremala, ufundi bomba, na taaluma nyingine za ufundi. Kwa mujibu wa Sora, kushiriki katika taaluma hizi sio tu kupata ajira, bali pia kunasaidia kuwaepusha vijana na matumizi ya dawa za kulevya. “Tumepiga hatua kubwa hadi sasa. Zaidi ya vijana 5,000 wamepata mafunzo mbalimbali katika kituo chetu, na wengi wao wanafanikiwa katika taaluma zao. Nawasihi vijana wengi zaidi waje katika kituo chetu ili wachangamkie fursa hizi badala ya kupoteza muda mitaani,” alisisitiza.
Mbali na kuwawezesha vijana, Sora pia aligusia umuhimu wa utunzaji wa mazingira. Aliangazia thamani ya taka za plastiki, akiwahimiza wakaazi wa pwani kuepuka kutupa taka ovyo na badala yake kuzikusanya kwa ajili ya urejeleaji. Kwa upande mwingine, Mike Odhiambo, msaidizi wa maabara katika kituo hicho cha I.O.ME 001,naye alieleza kuhusu juhudi za shirika hilo katika kukuza ubunifu, hasa miongoni mwa wanafunzi. “Kituo chetu kimewasaidia wanafunzi wengi wa vyuo vikuu wanaokuja hapa kufanya miradi yao ya kitaaluma bila malipo. Tunatoa jukwaa la utafiti na ubunifu kwa mtu yeyote aliye na hamu, bila kujali kiwango chake cha elimu,” alisema Odhiambo. Aliongeza kuwa kituo hicho kina mashine mbalimbali za kushona, kuchonga, pamoja na vifaa vya utafiti wa uhandisi na tiba, hivyo kuwapa vijana fursa ya kupata uzoefu wa vitendo.
I.O.ME 001 inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwawezesha vijana wengi, wenye ujuzi na wasio na ujuzi, katika Kaunti ya Mombasa na maeneo yote ya pwani. Katika siku zijazo, shirika hilo linapanga kupanua huduma zake hadi kaunti zingine ili kuongeza mafunzo kwa jamii. Kadri teknolojia inavyoendelea kubadilisha sekta mbalimbali, taaluma za ufundi zinaendelea kuwa suluhisho mwafaka kwa changamoto ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana. Wito uko wazi: vijana wanapaswa kufungua mawazo yao kwa fursa mpya na kuchangamkia nafasi zilizopo katika sekta za kazi za mikono na ujuzi wa kiufundi.
By Simon Cephas Mwalimu