Asilimia 45 ya wakazi ukanda wa pwani wanaugua kisukari hali ambayo imepelekea wengi kukumbwa na matatizo ya macho.
Wakazi wengi ukanda wa pwani wametajwa kukumbwa na maradhi aina mbili yanayochangia wao kukumbwa na matatizo ya macho.
Daktari David Sawe, mtaalam wa upasuaji wa macho katika kituo cha matibabu ya macho cha Light For Christ Eye Centre mjini Mombasa anasema ugonjwa wa kisukari na shinikizo ya damu kwenye macho ni maradhi yanayoathiri idadi kubwa ya wakazi kwenye macho.
Ameeleza kuwa idadi kubwa ya waathiriwa wa ugonjwa wa macho ukanda wa pwani ni wanaume.
“Tulikuwa tunashughulikia ugonjwa wa kisukari hasa unapoathiri ndani ya jicho. Na takwimu ambazo tukonazo ni kuwa asilimia 45 ya wakazi ukanda wa pwani wanaugua kisukari. Wengi wa wanalioathiriwa na ugonjwa huo ni wanaume.” Alisema Dkt. Sawe.
Aidha ametoa wito kwa wakazi ukanda wa pwani kuchukua hatua ya kujitokeza na kufanyiwa uchunguzi wa macho ili kuepuka kugundulika kwa ugonjwa huo ukiwa umeenea kwenye sehemu kubwa ya macho.
“Wameyapa kipaumbele mambo yaliyo kinyume cha afya zao. Yaani wamezingatia zaidi shughuli zao za kimaisha, kisha familia zao, Mungu na mwisho wanafikiria kuhusu afya zao. Lakini inapasa kuwa tunapeana kipaumbele Mungu kisha afya pamoja na familia zetu. Tukiwa na afya njema hapo tutaweza kufanya shughuli zetu kama vile kwenda kazi bila matatizo na tunafaa kufuata mfumo huo.” alisema Dkt. Sawe.
Hayo yamejiri kufuatia kituo cha matibabu ya macho cha Light For Christ Eye Centre kuandaa shughuli ya uchunguzi wa bure wa macho mjini Kilifi utakao fanyika kwa siku mbili.
Erickson Kadzeha