Wazazi kaunti ya Mombasa wamehimizwa kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya wana wao na kuwapa mwongozo ufaao wa malezi ili wanyooke kimaadili.
Ndio wito na ujumbe uliorindima katika hafla ya Iftar ya Wakfu wa Mama Haki makala ya 4 iliyoandaliwa kwa kwa waumini wa dini ya kiislamu katika kaunti ya Mombasa.
Mamia ya wakaazi wa eneo hilo walifurika katika uwanja wa Mwahima mapema Ijumaa kuhudhuria hafla hiyo ambako mengi yalikuwa yameandaliwa si burudani, mawaidha, ushauri nasaha na shinikizo kwa jamii kukumbatia elimu na malezi bora kwa watoto wao.
Akizungumza katika dhifa hiyo Seneta mteule wa Mombasa Miraj Abdillahi aliwahimiza wazazi kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya wanao na kuwapa mwongozo ufaao ili wanyooke kimaadili.
Miraj amesema vijana wa ukanda wa pwani wana nafasi sawia ya kuwa watu wa maana maishani iwapo watapewa motisha na mwongozo ufao.
“Wapwani vijana wa hapa Likoni, Mombasa na Pwani wana nafasi sawa za kiajira na maendeleo, zile fursa ziko pia mtoto wa hapa anayo fursa mara nyingi tunaona kuwa ni ndoto, tunaishia kusifiwa kuwa ni vijana wa mapanga na vijana wavivu, zile fursa ziko ulimwengu huu si fursa za watu kadhaa, bali fursa hizi ni za wote Pwani.”
Niwahimize wazazi kuzingatia malezi na elimu vijana wapate fursa hizi kujiendeleza.” akasema.
Kwa upande wake Prof. Dkt. Othman Mujahid ambaye alikuwa mzungumzaji mkuu wa hafla hiyo naye aliwatakawazazi wawe kielelezo chema kwa wanao akisema shule ya kwanza kwa watoto ni nyumbani wanakoishi.
Kadhalika amewahimiza wazazi kuendelea kuwapa mwongozo mwema na mafunzo ya maadili wanao pasi kuangazia umri wao akisema kwamba mwana kwa nina hakui.

“Ni sharti tuwalee watoto kwa mapenzi na tutanmbue kwamba malezi bora yatapatikana tu iwapo wazazi watakuwa na nidhamu na adabu ya hali ya juu. Watoto wetu hawasikilizi yale tunayowaambia wala kuwashauri bali wanatizama yale tunayoyafanya, wanajifunza yale wanayoyaona nyumbani kabla hata wapate elimu shuleni.”
Fauka ya hayo seneta Miraj alichukua fursa hiyo kuiomba jamii iwe na imani na bima mpya ya afya ya jamii nchini SHA.
Miraj amedokeza kuwa serikali kupitia wizara ya afya inafanya kila iwezalo kuhakikisha utendakazi wa bima hiyo ni shwari na kwamba kila mkenya anapata fursa ya kuhudumiwa si tu katika hospityali za rufaa na hata vituo vidogo vya afya.
“Na tunapozungumzia masuala ya uongozi, hata tukitekeleza miradi ya aina gani au hata tuzalishe nafasi za kazi, ni lazima jamii iwe na afya bora na ndio maana kupitia serikali ya Rais Ruto tumewashinikiza wananchi kujisajili katika bima mpya ya SHA,” Miraj alisema
Kauli hiyo imetiliwa pondo na seneta wa Mandera Mariam Omar ambaye amesema bima hiyo inazingatia usawa na kuwa kila mwananchi atapata fursa ya kupata huduma za afya pasi kubaguliwa kwa misingi ya kitabaka.

“Watu sahihi ambao waneza kueleza iwapo SHA inafanya kazi au la ni kamati ya afya nchini. Hivyo tunawaomba viongozi kote nchini watembelee vituo vya afya katika maeneo yeo ili wakathibitishe kama SHA inafanya kazi au La.” Mariam alieleza.
“SHA ni ya wanyonge, sisi kama viongozi tuna bima inayogharamia matibabu yetu lakini tumeafikiana kulipia SHA kwa ajili ya wananchi wasiojiweza, tafadhali jisajilini kwani hamuwezi kunaufaika na huduma za afya iwapo hamtajisajili.” Seneta Mariam aliongeza.
Dhifa hiyo iliaandaliwa kuwaleta pamoja waumini wa dini ya kiislam na jamii ya kaunti ya Mombasa ili kujadili masuala muhimu yanyoathiri jamii na kusisitiza haja ya kuwapa watoto malezi bora, kauli mbiu ya Dhifa ya mwaka huu makala ya 4 ikiwa ‘malezi bora na sio malezi bora.’
BY MWAJUBA MOHAMMED