HabariMazingiraMombasaNews

Serikali kuajiri maofisa elfu kumi kuimarisha usalama.

Serikali kuajiri maofisa elfu kumi kuimarisha usalama.

Serikali imesema imeweka mpango wa kimakakati kwa kuajiri maofisa elfu kumi kama njia ya kuzidi kuimarisha usalama kote nchini, hatua hiyo inaonyesha jinsi swala la usalama linavyochukuliwa kwa uzito.

Waziri wa usalama wa ndani Kipchumba Murkomen amesema serikali itawaajiri maofisa wa polisi elfu kumi katika kipindi cha miezi mitatu ili kuimarisha usalama, katika maeneo ambayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto ya utovu wa usalama.

Akizungumza katika kikao cha baraza la usalama mjini Kilifi waziri huyo ameeleza kuwa maofisa wa polisi wamekuwa wakipitia wakati mgumu kushika doria katika baadhi ya maeneo kutokana na uchache wa maofisa hao huku akiongeza kuwa swala hilo limepelekea maofisa wengi kusalia eneo moja kwa muda mrefu.

“Tunakusudia kuajiri polisi elfu kumi katika miezi mitatu ili kuhakikisha kuwa vituo vya polisi vinakuwa na uzito unaostahili. Na sisi kama serikali tumehakikisha kuwa kuna uboreshaji katika maofisa wa polisi. Na mambo ya kubadilisha vituo vya maofisa wa polisi wanapohudumutukiwa na polisi wachache inatupa changamoto hasa katika operasheni maalum. Ila changamoto kubwa zaidi ni idadi ndogo ya maofisa wa polisi.” alisema Murkomen.

Aidha amebainisha kuwa katika kuimarisha usalama serikali inapanga kununua magari elfu 5 yatakayosaidia maofisa wa polisi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Matakwa ya maofisa wetu wa polisi kote nchini pamoja na maofisa tawala ni kitu ambacho kina uzito mkubwa. Na shida iliyopo hapa mashinani ni ukosefu wa magari, nusu ya vituo vya polisi kote nchini havina magari na nia yetu ni kuhakikisha kwamba tumewatafutia magari. Na tayari mpango wa ununuzi unaendelea katika hazina ya kitaifa tukijaribu kununua magari elfu 5. Na hayo magari tukiyapata tutayagawana kidogo kidogo kwa maofisa wa polisi na mengine kwa maofisa wa magereza pamoja na maofisa tawala.” alisema Murkomen.

Kwa upande wake mbunge wa Malindi Amina Mnyazi ameeleza kuwapo kwa changamoto ya uhaba wa  maofisa wa polisi na magari eneo hilo akisistiza kuwa uhaba huo umechangia kuibuka kwa magenge ya vijana ya uhalifu.

“Malindi ikiwa miongoni mwa miji maarufu sana kaunti ya Kilifi inasikitisha kule Malindi niko na kituo cha polisi ambayo nafikiria wale wafanyakazi pale ni wachache hawazidi 120. Sijui “ratio” ni gani kati ya askari na wananchi lakini nikiangalia ile idadi ya watu wangu wa Malindi dhidi ya maofisa wa polisi 120 naona hao maofisa ni wachache na tunahitaji kuongezewa watu ili waweze kufanya kazi vizuri. Askari wa trafiki, OCS na askari wa kulinda watalii wote hawana magari jambo hilo linawatatiza katika utoaji huduma kwa wananchi.” alisema Mnyazi

Erickson Kadzeha.