HabariLifestyleMombasaNews

Jamaa mmoja afariki dunia baada ya kugongwa na mwakilishi wadi.

Jamaa mmoja amefariki dunia papo hapo eneo la Kilodi wadi ya Matsangoni katika barabara kuu ya Mombasa Malindi baada ya kugongwa na gari lililokuwa likiendeshwa na wawakilishi wadi katika bunge la kaunti ya Kilifi.

Kulingana na Juma Chengo mwakilishi wadi wa Mnarani wawakilishi wadi hao walikuwa wanaelekea mjini Malindi mwendo wa saa tatu asubuhi kwa vikao vya uchukuzi wa kaunti ya Kilifi  wakati gari hilo aina ya Toyota Fielder lililokuwa likiendeshwa na mwakilishi wadi wa Mwarakaya Stanley Mkadi lilipopoteza mwelekeo lilipokuwa likijiaribu kupita gari jingine kuelekea Malindi na kugongana ana kwa ana na mwendeshaji pikipiki ambae alifariki dunia papo hapo.

“Tulikuwa tunasafiri bungeni kwa kikao cha uchukuzi wa kaunti nikiwa na mwenyekiti wa kamati hiyo ya uchukuzi na aliyepia mwakilishi wadi wa Mwarakaya Stanley Mkadi sasa tulipofika hiyo sehemu ndipo tukahusika kwenye hiyo ajali.” alisema Chengo.

Kamanda wa polisi eneo bunge la Kilifi kaskazini Stanley Tonui amethibitisha kisa hicho huku akiwataka madereva kuwa waangalifu wanapotumia barabara ili kutohatarisha usalama wa watumizi wengine wa barabara.

Aidha ameeleza kuwa tayari polisi wameanzisha uchunguzi wa kiini cha ajali hiyo.

“Imetokea wakati alipokuwa akiendesha gari lake akielea upande wa Malindi na alipokuwa akilipita gari jengine likagongana ana kwa ana na mwendeshaji pikipiki ambapo mwendeshaji pikipiki huyo akaaga dunia. Kwa sasa uchunguzi unaendelea ila ningependa kuwasihi madereva na watumizi wengine wa barabara kuwa makini ili wasihatarishe maisha ya watumizi wengine wa barabara.” alisema Tonui.

Ikumbukwe ni visa vitatu vya ajali ambavyo vimeripotiwa katika eneo hilo katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Erickson Kadzeha.