Suala la uhaba wa wafanyakazi katika taasisi muhimu za
serikali ya kaunti ya Mombasa limetajwa kuwa kikwazo
kinachopelekea kulemaa na hata kukosekana kwa
huduma muhimu na mwafaka.
Haya yamebainika wakati wa uzinduzi wa ripoti ya uangalizi wa
utendakazi wa kaunti iliyofanywa na Afisi ya Seneta wa Mombasa
Mohammed Faki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo ya Uangalizi wa
Kaunti ya mwaka wa kifedha 2022/2023, 2023/2024 na 2024/25
Seneta wa Mombasa Mohammed Faki, amebaini suala hilo
kuwa kikwazo kinachowanyima wakazi wa Mombasa haki ya
kupata huduma kwa wakati.
Akipigia mfano suala la hivi punde la kuporomoka kwa jumba la
ghorofa 10 Seneta Faki amesema kutokea kwa kisa hicho ni
ishara wazi kuwa hali ya ukaguzi wa majengo mjini Mombasa
imedorora kutokana na uhaba wa maafisa husika hasa wahandisi
wa kufika nyanjani kufanya ukaguzi huo.
“Tumeshuhudia matukio mawili katika kipiindi cha wiki mbili
ikiwemo kuporomoka kwa lile jumba la ghorofa na hii ni ishara
kwamba hatufanyi vyema katika idara husika.
Idara ya ukaguzi wa majumba ina uhaba mkubwa wa maafisa
ikiwemo wahandisi na wakaguzi na iwapo suala hili
halitaangaziwa basi tutakuw akatika hatari ya kukumbwa na
majanga kama haya katika siku zijazo,” alisema Seneta Faki.
Kwenye ripoti hiyo Seneta Faki pia amebaini kuwa Kaunti inakosa
fursa mwafaka za kuendeleza sekta mbalimbali kutokana na
kukosa mipango mwafaka, kama vile mikakati ya kuwafadhili na
kuwaendeleza vijana kitaaluma katika taasisi na vyuo vya
kiufundi.
Seneta Faki vilevile ameutaka uongozi mkuu wa kaunti ya
Mombasa kuiangazia ripoti hiyo na kuifanyia kazi ili kurekebisha
matatizo na changamoto zilizoibuliwa, huku pia akilishinikiza
Bunge la kaunti hiyo kuwajibika vilivyo kwa kufuatilia uwajibikaji
na utendakazi wa kaunti kwa manufaa ya mkaazi wa Mombasa.
“Natoa wito kwa serikali ya kaunti ya Mombasa kuzinduka na
kuimarisha utendakazi wake kwa wakaazi na iwapo ripoti hii
itamgusa kiongozi yoyote basi afanye hima arekebishe ili
wananchi wapate huduma inavyostahiki.” Faki aliieleza.
Changamoto nyingine zilizotajwa na ripoti hiyo ni ukosefu wa
vifaa muhimu vya kazi katika vituo vya idara ya zimamoto,
ukosefu wa ambulensi, ubaguzi na upendeleo katiia kuajiri
wafanyakazi, kuchelewa kukamilika kwa miradi ya sekta na idara
zote za kaunti, na kutotumika vyema kwa fedha zilizotengewa
miradi husika.
Hata hivyo kaunti ya Mombasa imejitetea ikisema imejitahidi
vilivyo katika kufanikisha miradi yake na kwamba iko mbioni
kuhakikisha inatekeleza miradi yake kabla kukamilika muhula wa
uongozi wake Gavana.
Dkt. Mbwarali Kame ni Waziri wa Elimu kaunti ya Mombasa.
“Kama serikali ya kaunti ya Mombasa tumejitolea kuhakiksha
tunaangazia miradi yetu na utendakazi kwa wananchi
waliotuchagua.Tumefanya mengi kufikia sasa na tuna hakika
kwamba tutakamilisha miradi yetu kwa muda ufaao kama
alivyoahiidi Gavana AbdhulSwamad Shariff Nassir.”
Katika ripoti hiyo ya uangalizi wa utendakazi wa kaunti
iliyofanywa na Afisi ya Seneta wa Mombasa Mohammed Faki,
imeangazia masuala ya kaunti katika mwaka wa kifedha wa 2022-
2023, 2023/24 na 2024/25, na ilihusisha utafiti wa afisi ya seneta
huyo na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Na Mjomba Rashid