Suala la uhaba wa wafanyakazi katika taasisi muhimu za serikali ya kaunti ya Mombasa limetajwa kuwa kikwazo kinachopelekea kulemaa na hata kukosekana kwa huduma muhimu na mwafaka.
Haya yamebainika wakati wa uzinduzi wa ripoti ya uangalizi wa utendakazi wa kaunti iliyofanywa na Afisi ya Seneta wa Mombasa Mohammed Faki.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo ya Uangalizi wa Kaunti ya mwaka wa kifedha 2022/2023, 2023/2024 na 2024/25 Seneta wa Mombasa Mohammed Faki, amebaini suala hilo kuwa kikwazo kinachowanyima wakazi wa Mombasa haki ya kupata huduma kwa wakati.
Akipigia mfano suala la hivi punde la kuporomoka kwa jumba la ghorofa 10 Seneta Faki amesema kutokea kwa kisa hicho ni ishara wazi kuwa hali ya ukaguzi wa majengo mjini Mombasa imedorora kutokana na uhaba wa maafisa husika hasa wahandisi wa kufika nyanjani kufanya ukaguzi huo.
“Tumeshuhudia matukio mawili katika kipiindi cha wiki mbili ikiwemo kuporomoka kwa lile jumba la ghorofa na hii ni ishara kwamba hatufanyi vyema katika idara husika.
Idara ya ukaguzi wa majumba ina uhaba mkubwa wa maafisa ikiwemo wahandisi na wakaguzi na iwapo suala hili halitaangaziwa basi tutakuw akatika hatari ya kukumbwa na majanga kama haya katika siku zijazo,” alisema Seneta Faki.
Kwenye ripoti hiyo Seneta Faki pia amebaini kuwa Kaunti inakosa fursa mwafaka za kuendeleza sekta mbalimbali kutokana na kukosa mipango mwafaka, kama vile mikakati ya kuwafadhili na kuwaendeleza vijana kitaaluma katika taasisi na vyuo vya kiufundi.
Seneta Faki vilevile ameutaka uongozi mkuu wa kaunti ya Mombasa kuiangazia ripoti hiyo na kuifanyia kazi ili kurekebisha matatizo na changamoto zilizoibuliwa, huku pia akilishinikiza Bunge la kaunti hiyo kuwajibika vilivyo kwa kufuatilia uwajibikaji na utendakazi wa kaunti kwa manufaa ya mkaazi wa Mombasa.
“Natoa wito kwa serikali ya kaunti ya Mombasa kuzinduka na kuimarisha utendakazi wake kwa wakaazi na iwapo ripoti hii itamgusa kiongozi yoyote basi afanye hima arekebishe ili wananchi wapate huduma inavyostahiki.” Faki aliieleza.
Changamoto nyingine zilizotajwa na ripoti hiyo ni ukosefu wa vifaa muhimu vya kazi katika vituo vya idara ya zimamoto, ukosefu wa ambulensi, ubaguzi na upendeleo katiia kuajiri wafanyakazi, kuchelewa kukamilika kwa miradi ya sekta na idara zote za kaunti, na kutotumika vyema kwa fedha zilizotengewa miradi husika.
Hata hivyo kaunti ya Mombasa imejitetea ikisema imejitahidi vilivyo katika kufanikisha miradi yake na kwamba iko mbioni kuhakikisha inatekeleza miradi yake kabla kukamilika muhula wa uongozi wake Gavana.
Dkt. Mbwarali Kame ni Waziri wa Elimu kaunti ya Mombasa.
“Kama serikali ya kaunti ya Mombasa tumejitolea kuhakiksha tunaangazia miradi yetu na utendakazi kwa wananchi waliotuchagua.Tumefanya mengi kufikia sasa na tuna hakika kwamba tutakamilisha miradi yetu kwa muda ufaao kama alivyoahiidi Gavana AbdhulSwamad Shariff Nassir.”
Katika ripoti hiyo ya uangalizi wa utendakazi wa kaunti iliyofanywa na Afisi ya Seneta wa Mombasa Mohammed Faki, imeangazia masuala ya kaunti katika mwaka wa kifedha wa 2022-2023, 2023/24 na 2024/25, na ilihusisha utafiti wa afisi ya seneta huyo na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Na Mjomba Rashid