HabariNews

Matatizo ya afya ya akili ni tishio la usalama Kilifi

Matatizo ya afya ya akili yakiendelea kuwatatiza maelfu ya wakazi humu nchini, mikakati imewekwa wadi ya Mnarani kaunti ya Kilifi kukabiliana na changamoto ya kiusalama inayotokana na watu walio na tatizo la afya ya akili.

Kwa mujibu wa mwakilishi wadi ya Mnarani Juma Chengo, visa kadhaa vya watu walio na matatizo ya afya ya akili kuwavamia na kuwashambulia wakazi vimekuwa vikishuhudiwa jambo analohisi linahatarisha usalama wa wakazi.

Ameeleza kuwa tayari vijana kadhaa katika kijiji cha Takaungu wamepelekwa kwenye taasisi za kuwasaidia watu wanaokumbwa na matatizo ya akili katika mpango wa kukabiliana na changamoto hiyo inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na utumizi wa dawa za kulevya pamoja na kuhakikisha kuwa kuna usalama wa kutosha kwa wakazi.

Tumeamua kuwapeleka “Rehab” wale ambao wanamatatizo ya afya ya akili ikiwa hatua hii ni kutokana na kisa cha kuogopesha cha mauaji cha hivi majuzi hapa kijijini kwetu ambacho sichakawaida. Lakini baada ya kuchunguzwa ilibainika kwamba yule kijana alikuwa na matatizo ya afya ya akili.” alisema Chengo.

Chengo amebainisha kuwa vijana zaidi ya watano tayari wamenufaika na mpango huo, huku akieleza kuwa pindi vijana hao watakaporuhusiwa kurudi nyumbani watatafutiwa kazi ili kuwaepusha kurudia nyendo zao za zamani.

Hata hivyo amewasihi wakazi kutowaficha jamaa zao walio na matatizo hayo ya afya ya akili ili waweza kupata usaidizi.

Nakumbuka watu watano ambao tumewapeleka na wengine wengi mmoja baada ya mwengine ili wasaidike. Na hivi sasa tumepanga na wafadhili wengine kama vile Mombasa Cement kupitia Imtiaz Sayani kwamba tukiwapeleka “Rehab” watakaporudi tutawapa vibarua ili wazidi kurekebishika zaidi. Pia natoa wito wangu kwa wakazi kote nchini kutowaficha jamaa zao walio na matatizo ya akili, tafadhali wawatoe na kuwapeleka “Rehab” ili wasaidike.” alisema Chengo.

Ikumbukwe ni chini ya majuma matatu tangu kufanyika kwa kisa cha kuogofya katika kijiji cha Takaungu ambapo kijana mmoja anadaiwa kumvamia na kumuua mzee na kisha kula utumbo wake.

Erickson Kadzeha