HabariNews

Vita dhidi ya dhulma za kijinsia na unyanyasaji wa kingono kwa watoto vyapigwa jeki Kilifi

Vita dhidi ya dhulma za kijinsia na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake na watoto vimepigwa jeki eneo la Gede kaunti ya Kilifi kufuatia kuzinduliwa kwa ofisi maalum ya kushughulikia kesi hizo maarufu “Safe Space” katika kituo cha polisi cha Gede.

Ukanda wa pwani ukiwa miongoni mwa maeneo yanayoshuhudia visa vingi vya dhulma za kijinsia na unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto, mikakati inaendelea kuwekwa ili kukabiliana na ongezeko la visa hivyo.

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa mradi wa kukabiliana na visa vya dhulma za kijinsia na unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake na watoto katika shirika la International Justice Mission IJM Aggrey Juma, kuzinduliwa kwa ofisi hizo maalum katika baadhi ya vituo vya polisi zitasaidia waathiriwa kujihisi huru na kutoa taarifa pasi hofu ya kunyanyapaliwa, pamoja na kuwa faragha kwa waathiriwa wakati wa kuhudumiwa na maofisa wa polisi wanaosimamia vituo vya jinsia.

Siku ya leo tumezindua ofisi maalum ”child friendly space” katika kituo cha polisi cha Gede ambapo kwa muda mrefu hapajakuwa na ofisi tangu mwaka 2021 maofisa wa polisi wanaoshughulikia kesi za dhulma dhidi ya watoto walikuwa wakiketi chini ya mti ili kushughulikia kesi hizo ndipo tukaona ni vyema tufanye jambo.

“Tuliwaletea hema lakini hatukuishia hapo kwasababu kituo hiki kinashughulikia kesi nyingi sana za watoto ndiposa tumeleta ofisi hii ambayo inavifaa muhimu na pia inaweka mazingira yanayovutia kwa watoto na pia kuleta hali ya faragha kwa waathiriwa.” alisema Juma.

Hakimu mkuu katika mahakama ya Malindi Elizabeth Usui ameeleza kuwa tayari visa 115 vya unyanyasaji wa kingono dhidi watoto eneo la Gede na Malindi vimeripotiwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu 2024 hadi kufikia mwezi Novemba mwaka huu.

Amebainisha kuwa idara ya mahakama inajizatiti iwezavyo kuzishughulikia kesi hizo kwa muda mfupi iwezekanavyo akieleza kuwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu kesi za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto huwa zishaamuliwa.

Usui ametoa wito kwa wazazi kuwa waangalifu na kuwachunga watoto wao hasa msimu huu wa likizo ndefu ambapo visa vingi hushuhudiwa.

Kesi nyingi ambazo tunazipata pale kortini ni zile tunaziiita unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto na kufikia sasa tumepokea visa 115 tangu mwanzoni mwa mwaka huu 2024 mpaka kufikia mwezi huu wa Novemba na bado mwaka haujaisha na tunazidi kuandikisha visa hivi.

“Kwa wakati huu shule zimefungwa na haya madhara ndio yanafanyika zaidi basi ningewaomba wazazi wachunge watoto wasiwaruhusu kwenda kwa disko matanga kwasababu hapo ndipo maovu yote yanapoanzia.” alisema Usui.

Kamanda wa polisi kaunti ya Kilifi Joseph Ongaya ameisihi jamii kuweka mazingira bora kwa watoto na kujitenga mbali na mila na desturi potofu za unyanyasaji wa watoto.

Nataka nisistize, tuangalie kwa upana na marefu ni nani ambae tunafaa kumfikiria zaidi? Naisihi jamii yetu ya upande huu, naisihi jamii yetu tukiwa Wakenya tuangalie tuliko toka na tuwe na hofu ya Mungu. Natumuangalie mtoto, huyu mwathiriwa kila mtu mwenye utu katika dunia hii lazima tuwape kipaumbele waathiriwa, huyo mtoto mdogo. Nawaomba pale mahali ambapo tulipata kuna makosa hapo awali tuparekebishe kwasababu baada ya yote hayo tunataka watoto wa Kenya wapate mazingira bora na salama ya kuishi.” alisema Ongaya.     

Ikumbukwe hadi kufikia sasa IJM imefanikiwa kuzindua ofisi tatu maalum yaani “safe spaces” katika vituo vya polisi eneo la Bamburi, Msambweni na Gede.

Erickson Kadzeha