Katibu Mkuu wa masuala ya Bandari mjini Mombasa, Shadrack Mwadime amepuuzilia mbali kasumba kuwa wapwani wamekuwa wakikwepa masomo na kozi ngumu.
Akizungumza na wanahabari katika Kongamano la Vijana kuhusu Usafiri wa baharini, Mwadime alisema kwa sasa takwimu zinaonyesha vijana wa eneo hili wamepiga hatua katika masomo magumu kama vile uhandisi na masomo mbalimbali.
“Kasumba iliyokuwepo kwamba wapwani hawawezi kusomea masomo magumu ama hawasomi ati ni wavivu hapo zamani, ni uongo sasa. Uchumi wa Mombasa miaka themani na tisini kama unakumbuka vyema uliendeshwa na mabaharia.” Alisema.
Akiipinga vikali kasumba hiyo iliyodumu kwa muda sasa, Mwadime alisema kwa sasa pwani iko na uwezo wa kukusanya vijana kutoka maeneo mbalimbali kwa majengo ya kisasa yanayotumika kwa kutoa mafunzo kwa vijana.
“Mabaharia ndio walikuwa wakiongoza kwa ujenzi wa majumba kote hapa Pwani, wakiendesha uchumi wa Pwani. Ikiwa kasumba hii ilijengwa wakati huo lazima tuiondoe sasa na tuepukane nayo maana Wapwani wamesoma na lazima tuwaambie vijana wetu tuna mfumo wa kufuata na kuwaonyesha vijana wetu kuwa lazima kasumba hii tuiondoe,” alisema Mwadime.
Vile vile alisema hatua hiyo itawezesha kutoa nafasi za ajira miongoni mwa vijana huku akitoa wito kwa taasisi mbalimbali za elimu kuwaelimisha vijana kuhusu kilimo samawati.
“Tunafahamu ni kweli kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kiko juu sana na tunajua ukweli asilimia 75 ya idadi ya watu nchini ni vijana ilivyo sasa. Na hivyo ni lazima tuhakikishe kuwa jamii ya vijana wetu inahusishwa vilivyo na mahali pa kujihusisha napo ni sekta ya Uchumi Samawati, inabidi tuwavutie vijana wetu waone kuwa umuhimu na manufaa yaliyopo sekta hii ni makubwa sana.” Alisema.
Mwadime aidha alipendekeza iwapo watashirikiana na Idara ya Kitaifa ya maendeleo ya Vijana ili kuwezesha vijana kuingilia na kujihusisha katika biashara ya sekta hiyo.
BY EDITORIAL DESK