Serikali ya kaunti ya Mombasa imeweka mikakati mwafaka ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kukumbatia mbinu za kisasa katika sekta ya uchukuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari hapa baada ya kutia saini mkataba wa makubaliano na wadau mbalimbali Gavana wa kaunti hiyo Abdulswamad Sharrif Nassir amesema hatua hiyo mojawapo ya mikakati inayolenga kukabiliana na uchafuzi wa mazingira unaopelekea athari kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Kiuhalisia mkataba huu ni kutupa hakikisho katika upande wetu na washikadau kama kaunti kwamba tutaunga mkono mpango wa Kawi ya Kijani na kuweza kusaidia viwango vya utoaji nishati salama, na aidha kutoa nafasi kwa taasisi zetu za TVETs kutumika kama vituo vya kutoa mafunzo kwa hawa watkaokuwa wakiunda Tuktuk za umeme,” alisema Nassir.
Kwa upande wake Waziri wa Maji na Mali Asili kaunti ya Mombasa Emily Ochieng ameeleza baadhi ya manufaa yanayotokana na kukumbatia aina hiyo ya usafiri ikiwemo kubuni nafasi zaidi za ajira.
Aidha ameongeza kuwa wanapania kujenga kiwanda cha kutengeneza battery ili kuwafanyia wepesi na nafuu madereva wa aina hii ya usafiri kaunti hiyo.
“Kama kaunti tumekuwa jukumu kubwa katika sekta yetu ya uchukuzi inakumbatia mpango wa Kawi ya Kijani na salama kwani sekta hii ina mchango mkubwa hasi katika uchafuzi wa mazingira, na pia ina athari kuu za kiuchumi hasa kwa madereva kwa sababu ukilinganisha na ada zinazotozwa katika magari ya umeme dhidi ya kununua Dizeli ama Petroli iko juu kuliko umeme na tunataka kuhimiza mpito huo Kwenda kwa kwa utumizi wa uchukuzi wa vyombo vya usafiri vya kutumia umeme,” alisema.
Haya yanajiri baada serikali ya kaunti ya Mombasa kutia sahihi mkataba wa makubaliano baina yao na mashirika mbalimbali katika sekta ya uchukuzi na mazingira katika harakati ya kufanikisha lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
BY RASHID & BEBI SHEMAWIA