Kesi imewasilishwa mahakamani kupinga kuendelea kwa mtaala wa umilisi wa CBC uliochukua nafasi ya mfumo wa 8-4-4 .
Kupitia wakili Nelson Havi ,mlalamishi Esther Awour Adero amesema kuwa hatua ya wizara ya elimu kutekeleza mtaala mpya ni kunyume cha sheria na inaathiri mustakabali wa watoto kwa hivyo unapaswa kusimamishwa.
katika hati ya kiapo wakili Havi amesema kwamba kuna kilio kikubwa kutoka kwa umma ya jinsi mtaala huo wa CBC unatekelezwa bila kufuata sheria zinazotumika katika elimu ya msingi.
Havi amesema kukosekana kwa uwakilishaji wa wadau wote, watoto wanalazimika kufanya uamuzi wa kazi wanazozitaka kabla ya kupata maarifa, na jumla ya mafunzo yanayostahili ili kuwajuza kwa njia mwafaka itakayowafaa na kusema kuwa mtaala huo umeongeza mzigo wa kiuchumi wa kununua vitabu vya kozi na vifaa vingine vya kusomea.
Katibu wa Baraza la Mawaziri la maswala yanayohusiana na Elimu ya Msingi, Taasisi ya Maendeleo ya Mitaala ya elimu KICD, Baraza la Mitihani nchini, Tume ya kuajiri walimu TSC, Umoja wa Kitaifa wa Walimu wa Kenya, Bunge la Kitaifa, waziri wa usalama wa ndani Dk Fred Matiang’i na waziri wa elimu Profesa George Magoha wameorodheshwa kuhojiwa katika kesi hiyo.
BY NEWS DESK