Muungano wa walimu wa sekondari na vyuo vya kati nchini KUPPET, kaunti ya Kilifi umetoa makataa ya wiki mbili kwa tume ya kuajiri walimu nchini TSC kumpa uhamisho mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya St. Thomas la sivyo waandamane.
Kwa mujibu wa katibu wa muungano wa walimu wa shule za sekondari na vyuo vya kati nchini KUPPET, kaunti ya Kilifi Caleb Mogere, walimu shuleni humo wamekosa uhuru wa kufanya kazi kwa madai ya kunyanyaswa na mwalimu mkuu.
Naibu mwenyekiti wa muungano huo kaunti ya Kilifi Michael Mutuku anasema juhudi za kuboresha na kuinua viwango vya elimu kaunti hiyo havifai kuhujumiwa kwa faida ya mtu binafsi.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya St.Thomas mjini Kilifi Eunice Mwaiseghe, amekashifu madai ya viongozi wa muungano huo na kusema kuwa madai hayo hayana ukweli wowote.
Aidha amesistiza kuwa walimu wavivu wamekuwa na hulka ya kuwachochea walimu wengine ili kuhujumu shughuli za masomo shuleni humo.
BY ERICKSON KADZEHA