HabariNews

MUUNGANO WA JUMUIA YA KAUNTI ZA PWANI KUFANYIWA TATHIMINI.

Ikiwa ni takriban miaka 7 tangu kuundwa kwa muungano wa jumuia ya kaunti
za pwani, wadau mbali mbali sasa wanataka tathmini ifanywe ili kubainika
kwa hatua iliyopiga muungano huo katika kufanikisha ruwaza ya mwaka
2030.

Miongoni mwa ajenda kuu zilizopewa kipaumbele na muungano wa jumuia ya
kaunti za pwani tangu kuundwa kwake ni upatiakanaji wa chakula na lishe
bora katika kaunti zilizo kwenye muungano huo ruwaza ambayo ilifaa
kutekelezwa katika kipindi cha miaka 13, jambo ambalo lingeweza
kufanikiwa kwa kutumia mbinu ya kuwekeza zaidi kwenye uvuvi, uchumi wa
majini maarufu blue economy na ufugaji ng’ombe wa maziwa.

Mshirikishi wa mipango ya maendeleo katika jamii kaunti ya Kilifi Baha
Nguma, anasema viwango vya umaskini katika kaunti za muungano huu ni
asilimia 40.5 huku ikiwa lengo kuu ni kupunguza viwango hivyo hadi
asilimia 20 ifikapo mwaka 2030 hatua inayoweza kufanikishwa kwa kuunda
nafasi milioni moja za ajira.

Hata hivyo Nguma anasema huenda kukawa na changamoto ya kutimiza azma ya
muungano wa jumuia ya kaunti za pwani ifikapo mwaka 2030 kutokana na
ulegevu wa viongozi kupitisha sheria ya kuundwa kwa hazina
itakayosimamia shughuli za muungano huo.

Ametoa wito kwa magavana kwenye muungano wa jumuia ya kaunti za pwani
kupitia mwenyekiti wake Gedion Mung’aro ambaye pia ni gavana wa Kilifi
pamoja na madiwani kulitilia pondo swala hili kwa kupitisha sheria
maarufu “Economic Block Act” katika mabunge ya kaunti mapema ili azma za
muungano huo ziweze kufikiwa ifikapo mwaka 2030.

BY ERICKSON KADZEHA.