Wanachama wote wa UDA kaunti ya Mombasa wametakiwa kuwa na ushirikiano kwa ajili ya manufaa na ustawi wa chama hicho.
Mshauri wa Rais katika maswala ya kisiasa Karisa Nzai, aliyasema haya alipokuwa kitoa hundi ya Basari eneo la Jomvu. Nzai aliwataka wanachama hao kuwa na umoja na kushirikiana akisema chama ni kimoja na hawataruhusu kuwa na migawanyiko chamani humo.
Kumekuwa kukishuhudiwa vuta nikuvute baina ya mbunge wa Nyali Mohammed Ali na aliyekuwa akiwania kiti cha Ugavana Kaunti ya Mombasa Hassan Omar Sarai jambo lililopelekea mgawanyiko wa wafuasi katika chama hicho.
Nzai hata hivyo aliwataka wafuasi wanaoegemea upande wa Mohammed Ali na wale wa Naibu mwenyekiti wa chama hicho Hassan Sarai kuwa waadilifu na kutochochea migawanyiko kwenye chama hicho.
“Wawe na ushirika umoja chama ni kimoja hatutaweza kuwa na watu amba wanaenda wakikosana hapa na pale na nyinyi wafuasi lazima makini msichochee migawanyiko tuweni na umoja” Alisema Nzai.
Wakati huo huo Nzai alidokeza juhudi za Rais William Ruto za kushusha gharama ya maisha akiwahimiza Wakenya kujihusisha na ukulima kama njia moja ya kushusha gharama hio huku akiwarai viongozi waliomamlakani kukoma kutoa maneno yanayokatisha matumaini kwa wananchi.
“Nataka kuwaambia wakenya Rais amejaribu vile awezavyo ni sisi tujishughulishe na ukulima hapo ndipo bei ya chakula itashuka ata pia nataka kuwaambia viongozi wenzangu wacheni kuropokaropoka maneno.” Alisema Nzai.
Kwa upande mwingine joseph Lena, Mshauri wa Nzai alipongeza mpango wa utaoaji basari kwa wanafunzi huku akiwarai wananchi kuwa subra na kumpa muda Rais Ruto akidokeza kuwa serikali ya Kenya Kwanza ilichukua uongozi wakati taifa lilikuwa linakumbwa na changamoto ya uhaba wa fedha.
“Wananchi wajipange mahali amejaribu jamaeni tumpe nafasi tuone atafikisha taifa wapi tusemeni ukweli aliwachiwa Kenya ikiwa pabaya.” Alisema Lena.