Kinara wa upinzani Raila Odinga Jumatatu Novemba 27, alikosoa serikali kuhusu dosari zilizorekodiwa katika matokeo ya mtihani wa Cheti cha Elimu ya Msingi ya 2023 (KCPE) yaliyotolewa hivi majuzi.
Matokeo yaliyotolewa na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu siku ya Alhamisi yalishuhudia malalamiko kutokana na mkanganyiko wa alama za baadhi ya watahiniwa katika Lugha Kiswahili na ile ya Ishara ya Kenya, somo wanalolidai kutolikalia katika mtihani huo.
Haya yanajiri huku Wazazi wa watahiniwa wa mtihani wa darasa la nane katika shule ya Saint GreenHill Academy jijini Nairobi wakilitaka baraza la mitihani ya kitaifa KNEC kusitisha zoezi hilo kufuatia wanafunzi wa shule hiyo kueleza kutoridhishwa na mbinu ambayo ilitumiwa na baraza hilo katika usahihishaji wa mitihani.
Haya ni baada ya wazazi na watahiniwa hao kusema kwamba waliona tofauti kubwa katika matokeo KCPE ya miaka ya awali na haya ya sasa jambo lililopelekea baadhi yao kufika mahakamani na kupinga uteuzi wa wanfunzi hao.
Shughuli hiyo ya uteuzi hata hivyo ilianza Novemba 27, na inatarajiwa kutamatika baada ya wiki mbili.