HabariLifestyleMombasa

Rais Ruto aonya wachochezi; aapa kukabiliana na ukosefu wa usalama kaunti ya Lamu

Rais William Ruto ameahidi kuwa Serikali itajizatiti vilivyo kuhakikisha suala la ukosefu wa usalama katika kaunti ya Lamu linatatuliwa kikamilifu.Akizungumza katika mkutano na viongozi kutoka kaunti ya Lamu katika ikulu ya rais jijini Nairobi Rais Ruto amewaomba viongozi wa eneo hilo kuungana na kufanya kazi kwa pamoja akisema mgawanyiko wowote unaotokea kati yao huwapa fursa magaidi kuendeleza ajenda zao za uharibifu.

Rais Ruto ametoa onyo kali kwa wote wanaotoa semi za uchochezi kwa wakaazi wa eneo hilo akisemna serikali haitomsaza yoyote.

“Ni lazima tuilinde Lamu; watu lazima waishi kwa amani kwa sababu wanastahili hivyo, matatizo ya Lamu hayako kwa wananchi yako kwa viongozi; nyinyi kama viongozi mtaamua Lamu iwe na usalama ama ugaidi.

Wakati sisi tunaelekeza mipango kupambana na magaidi pia hapa tuna shida ya uchochezi wa kisiasa ambayo inatuharibia usalama ya wananchi, tumechanganya matatizo ya ugaidi na matatizio ya uchochezi wa kisiasa ambayo inapiganisha wananchi,” alisema Rais.

Aliyasema hayo siku ya Alhamisi wakati wa mkutano na viongozi kutoka Kaunti hiyo katika Ikulu ya Nairobi.

Kiongozi wa Nchi alisema kuwa Serikali ina nia ya kuhakikisha kaunti hiyo itafungua uwezo wake wa kiuchumi, akitoa mfano wa biashara ya bandari ya eneo hilo.

Aliahidi kushughulikia umiliki wa ardhi na changamoto za maskwota zinazokabili Kaunti hiyo.

Kiongozi huyo wa Taifa aidha alitoa wito kwa viongozi kujiweka mbali na siasa za kujipendekeza kwa watu kwa gharama ya ajenda ya maendeleo ya nchi na kuwataka viongozi kutosita kufanya maamuzi ya kijasiri yenye maslahi kwa taifa la Kenya.

Naye Waziri wa usalama wa ndani Prof. Kithure Kindiki aliwataka viongozi wa kaunti ya Lamu kushirikiana ili kutoa hamasa kwa jamii dhidi ya uchochezi ambao ndio chanzo kikuu cha kuzorota kwa usalama katika kaunti hiyo.

“Changamoto tulizokuwa nazo ni uchochezi na kuingiza siasa katika masuala ya usalama, na tunafanya kila tuwezalo kukabiliana na kuhakikisha hakuna maafa yanashuhudiwa kwa wananchi na wanajeshi wetu huko. Ndugu zetu wa kisiasa wanaweza kutusaidia kwa kuongea na jamii huko Lamu ili wasiingie kwenye mtego wa magaidi ambao ni kugawanya wananchi na kuleta uhasama dhidi yao.” Alisema Kindiki

Kauli ya waziri Kindiki iliungwa mkono Gavana wa Lamu Issa Timami ambaye alisisitiza umuhimu wa hamasisho la umoja kwa jamii za eneo hilo na kutoa hakikisho kwamba atafanya kazi na viongozi wengine kufanikisha suala hilo.

“Kweli kuna masuala tata huko Lamu, kuna suala tata la wafugaji na wakulima lazima tutenge maeneo ya wakulima na wafugaji, wote ni Wakenya na wote wana haki. Lakini kwa niaba yangu na uongozi wa Lamu mheshimiwa Rais tutafanya kila tuwezalo ndani ya mamlaka yetu kuwaleta watu wetu pamoja, tuna mipango na tutakuja kukushirikisha na wewe tujadili,” alisema Gavana Timamy.

Viongozi waliohudhuria kikao hicho huko Ikulu ni pamoja na Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, Mawaziri Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani) na Aden Duale (Ulinzi), Katibu Mkuu wa Usalama wa Ndani Raymond Omollo, Gavana wa Kaunti ya Lamu Issa Timamy, wabunge Ruweida Obbo (Lamu Mashariki), Stanley Muthama (Lamu Magharibi), Joseph Githuku (Seneta, Lamu), Monica Muthoni (Mwakilishi wa Wanawake, Lamu) na Wawakilishi wa Wadi.

Ikumbukwe kuwa Kaunti ya Lamu imeendelea kushuhudia hali tata ya usalama kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara ya magaidi wanaodaiwa kuwa wanamgambo wa kundi la Al-Shabab.